Na Tatu Mohamed
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amelishauri Baraza la Vyama vya Siasa kuanzisha kamati maalum ya kushughulikia makosa ya kisiasa ili kuhakikisha masuala yanayohusu siasa yanachakatwa kwanza ndani ya mfumo wa kisiasa kabla ya kupelekwa katika mifumo mingine ya kisheria.
Kauli hiyo imekuja wakati wa uzinduzi wa uongozi mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa pamoja na nembo ya baraza hilo uliofanyika Oktoba 7, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mwabukusi amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na changamoto zinazoweza kujitokeza pale masuala ya kisiasa yanapotafsiriwa na kushughulikiwa kwa kutumia mifumo ya sheria za kawaida bila kuzingatia mazingira na lugha ya siasa.
Amesema siasa zina mazingira na lugha yake, hivyo ni muhimu kuwa na utaratibu unaowezesha masuala hayo kushughulikiwa kwa mtazamo wa kisiasa kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.

“Kwa sababu kuna changamoto kubwa sasa ambayo tusipokuwa makini, itakuwa vigumu kufanya siasa ukijaribu kuitumia siasa katika sheria za kawaida. Siasa zina lugha zake, zina mazingira yake,” amesema.
Amesema jambo jingine muhimu ni kujenga utamaduni wa kuvumiliana miongoni mwa vyama vya siasa, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa sababu ya kuwatenga au kuwachukia watu wenye mitazamo tofauti.
“Mu-accommodate mwenzako. Ukishajifunza ku-accommodate, atajifunza kuondoa ile hofu. Utagundua katika mia moja, kuna mawili mnaweza mkafanya pamoja vizuri kwa maslahi ya taifa,” amesema.
Mwabukusi amesema tofauti nyingi za kisiasa zinachangiwa na hofu kuliko tofauti za mawazo, hivyo viongozi wanapaswa kujifunza kusikilizana na kutafuta maeneo wanayoweza kushirikiana kwa maslahi ya taifa.
Amesema pia ni muhimu kusimamia ukweli na uwajibikaji katika uwanja wa siasa, akieleza kuwa kukubali makosa na kuonyesha utayari wa kuyarekebisha kunaweza kusaidia kurejesha matumaini ya wananchi.
“Kwenye taifa, hapa tulipokwenda, lazima tujifunze kusema ukweli. Kwa sababu tukisema ukweli, ni dalili za kuanza kuwajibika,” amesema.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, vyama vya siasa vimepewa dhamana na wananchi kutengeneza sera na kujiandaa kuongoza nchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha vyama vilivyosajiliwa vinaonekana vikifanya shughuli za kisiasa katika maeneo mbalimbali.
Amemshauri Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua dhidi ya vyama ambavyo havionekani katika majukwaa ya kisiasa.
“Moja ya kazi ya Baraza la Vyama ni kuvifuta vyama ambavyo hatuvioni (field) kwenye majukwaa,” amesema.
Amesema vyama havilazimiki kufanya shughuli za kisiasa katika kila eneo la nchi, bali vinaweza kuchagua maeneo machache yenye nguvu na kujenga ushawishi wake huko.
“Tambua nguvu yako, tafuta vijimbo vyako viwili, vitongoji vyako vinne vya madiwani, mwingine aende huku,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwabukusi ametoa wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuongeza usajili wa vyama vipya ili kutoa nafasi kwa kizazi kipya kushiriki katika siasa kupitia vyama vinavyowakilisha mitazamo na lugha yao.
Amesema kutokuwepo kwa nafasi hiyo kunaweza kuwafanya baadhi ya vijana kutafuta njia nyingine za kujieleza kisiasa, ikiwamo kuunda vikundi vya uasi.
“Msajili wa Vyama vya Siasa kuongeza usajili wa vyama, ongezeni vyama. Msipoongeza vyama, hawa vijana wataunda vitendo vya uasi. Wapeni lugha yao, waone kuna chama cha Gen Z kinakuja kinachoenda na lugha yao,” amesema.
Amesema hatua hiyo haimaanishi kila kundi lisajiliwe kuwa chama cha siasa, bali kuwe na fursa kwa makundi mapya yenye mawazo na mitazamo tofauti kushiriki katika mfumo rasmi wa kisiasa.
Mwabukusi amesema endapo vyama vitakuwa na nguvu katika maeneo mbalimbali ya nchi, ushindani wa kisiasa unaweza kusaidia kujenga mazingira ambayo vyama vitahitaji kukaa pamoja, kujadiliana na kufikia makubaliano katika masuala ya kitaifa.


