Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Profesa Palamagamba Kabudi, amevitaka vyama vya siasa nchini kuendelea kutumia mazungumzo na mashauriano katika kutatua tofauti zao na kujenga demokrasia, amani, utulivu na umoja wa kitaifa.
Profesa Kabudi amesema hayo leo Oktoba 07, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizindua uongozi mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa pamoja na nembo ya Baraza hilo.
Amesema mfumo wa vyama vingi vya siasa haupaswi kutafsiriwa kuwa uadui au uhasama, bali ni mfumo unaowapa Watanzania wenye mitazamo na mawazo tofauti nafasi ya kukaa pamoja, kujadiliana na kutoa mawazo kwa ajili ya mustakabali wa taifa.

“Mfumo wa vyama vingi ni kuwasaidia Watanzania wote wenye maoni tofauti na mawazo tofauti kukaa pamoja, kujadili na kuangalia mustakabali wa taifa lao. Sio uadui, sio uhasama, sio shari wala sio vitisho,” amesema.
Profesa Kabudi amesema utamaduni wa Tanzania wa kuzungumza, kushauriana na kutumia hekima na busara umekuwa miongoni mwa sababu zilizosaidia nchi kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa licha ya kuwa na tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na kijamii.
Amesema viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kuheshimu maoni ya vyama vingine na kuepuka lugha zinazoweza kuongeza migawanyiko katika jamii.
“Demokrasia ni kusikilizana. Mtu wa demokrasia ni yule anayeweza kushuka, kuwa mnyenyekevu na kusikiliza maoni ya aliye mdogo kabisa,” amesema.
Aidha, amesisitiza kuwa hakuna chama cha siasa chenye hadhi kubwa kuliko kingine kwa mujibu wa sheria, hivyo vyama vyote vinapaswa kuheshimiwa na kupewa nafasi ya kutoa mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Amesema vyama vidogo pia vina nafasi muhimu katika demokrasia kwa kuwa vinatoa mawazo mbadala na kusaidia kuwakilisha mitazamo mbalimbali ya wananchi.
“Ni muhimu kuheshimu misingi ya taifa letu; hakuna ubaguzi, hakuna ukabila na hakuna ubaguzi wa aina yoyote. Vyama vyote vina hadhi sawa na vina mchango katika uongozi wa taifa,” amesema.
Profesa Kabudi pia amelitaka Baraza la Vyama vya Siasa kutumia nafasi yake kuwa jukwaa la mazungumzo kwa vyama vyote, akisisitiza kuwa changamoto za kisiasa zinaweza kutatuliwa kupitia majadiliano.
Amevitaka vyama ambavyo vimekuwa vikisusia baadhi ya vikao vya baraza hilo kurejea na kutumia jukwaa hilo kujadili hoja zao.
“Baraza hili ni jukwaa mwafaka la kujadili hoja na changamoto zozote, hata zile zenye uzito mkubwa. Hakuna jambo lisilowezekana katika mazungumzo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amewapongeza viongozi wapya wa Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuamua kuzindua uongozi wao pamoja na nembo ya baraza hilo, akisema hatua hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi hiyo katika kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini.
Amesema Serikali itaendelea kuwezesha na kuratibu shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa jukumu la serikali si kudhibiti vyama vya siasa bali kuwezesha na kuratibu mazingira ya kisiasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Ali Khatib, amesema baraza hilo lilitokana na Mwafaka wa CCM na CUF uliosainiwa Oktoba 10, 2001, kwa lengo la kumaliza migogoro ya kisiasa Zanzibar na kujenga amani, demokrasia na maridhiano.
Amesema katika mkutano wa wadau wa siasa uliofanyika Zanzibar mwaka 2003, uliowahusisha vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa, iliazimiwa kuundwa kwa jukwaa la kitaifa litakalovishirikisha vyama vyote vya siasa na wadau wengine.

Kwa mujibu wa Khatib, baadaye jukwaa hilo lilirasimishwa kisheria na kuwa Baraza la Vyama vya Siasa kupitia marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258.
Amesema kwa sasa baraza hilo lina wajumbe kutoka vyama vya siasa vyenye usajili kamili na linaongozwa na mwenyekiti pamoja na makamu mwenyekiti, huku likiwa na kamati zinazosaidia utekelezaji wa majukumu yake.
Khatib amesema miongoni mwa majukumu ya baraza hilo ni kumshauri Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu migogoro inayojitokeza miongoni mwa vyama, kutoa ushauri kuhusu masuala yenye maslahi ya taifa yanayohusu vyama vya siasa na hali ya kisiasa nchini, pamoja na kutoa ushauri kuhusu sheria na kanuni zinazohusu vyama vya siasa.
Amesema tangu kuanzishwa kwake, baraza limefanikiwa kuwakutanisha viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine kujadili masuala ya demokrasia, amani, utulivu na maslahi ya taifa.
Ametaja pia ushiriki wa baraza katika mijadala ya wadau iliyosaidia kuibua masuala yaliyofanyiwa kazi na Kikosi Kazi cha Rais cha mwaka 2022 kuwa miongoni mwa mafanikio yake.
Khatib amesema changamoto kubwa iliyopo ni baadhi ya vyama kutoshiriki kikamilifu katika vikao vya baraza, akivitaka vyama hivyo kurejea na kutumia jukwaa hilo kuwasilisha hoja zao.
Naye Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema Ofisi ya Msajili itaendelea kuwa sekretarieti ya Baraza la Vyama vya Siasa na kuhakikisha inaratibu na kuwezesha utekelezaji wa shughuli za baraza hilo.

Amesema baraza limekuwa likitoa nafasi kwa vyama vya siasa kusikilizana na kutafuta suluhu katika masuala mbalimbali, jambo ambalo limekuwa likijenga kuaminiana na kuimarisha mahusiano licha ya kuwepo kwa ushindani wa kisiasa.
“Tuendelee kulijenga Baraza la Vyama vya Siasa liendelee kuwa mfano katika bara la Afrika. Utamaduni wa kujadiliana licha ya tofauti za kisiasa ni tunu inayostahili kulindwa na kuendelezwa,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Dk. Evaline Munisi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Baraza la Vyama vya Siasa katika kuimarisha mahusiano kati ya Serikali, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya kijamii.
Amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni kukamilika kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mahusiano baina ya Serikali na Makundi ya Kijamii wa mwaka 2026, ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku zijazo.

Dk. Munisi amewapongeza viongozi wapya wa baraza hilo na kuwataka kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa ili kuimarisha demokrasia, ushiriki wa kisiasa, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.


