RASILIMALI ZA BAHARI ZATOA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA UCHUMI WA BULUU

Na Tatu Mohamed

TANZANIA na nchi nyingine za Bahari ya Hindi Magharibi zimetakiwa kutumia rasilimali za baharini kuanzisha biashara zinazoweza kuvutia uwekezaji, kwa kuongeza thamani, kutumia teknolojia, kuboresha usafirishaji na kuimarisha upatikanaji wa masoko badala ya kutegemea zaidi uuzaji wa mazao ghafi.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa, amesema sekta za uvuvi, mwani, matango ya baharini na ufugaji wa viumbe vya majini zinaweza kuingiza mapato makubwa zaidi iwapo wawekezaji watawekeza katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani.

Amesema fursa hazipo katika uvunaji wa rasilimali za baharini pekee, bali pia katika kuzichakata, kuboresha teknolojia, kuimarisha mifumo ya usafirishaji na kuwaunganisha wazalishaji na masoko yenye thamani kubwa.

“Wafanyabiashara na waandaaji wa miradi wanahitaji msaada ili kuwa tayari kwa uwekezaji. Wafadhili wanahitaji mifumo inayoaminika ya mapato, utawala bora na Serikali zinahitaji kuweka mazingira wezeshi na yanayotabirika kwa biashara,” amesema Kwagilwa.

Amesema mifumo ya ufadhili wa pamoja, dhamana, mitaji yenye masharti nafuu na ubia kati ya Serikali na sekta binafsi inaweza kusaidia kupunguza hatari za uwekezaji na kuwezesha biashara zinazopata changamoto kupata mikopo ya kibiashara kupata mitaji.

Kwagilwa ameyasema hayo wakati wa kongamano la biashara kuhusu uwekezaji endelevu katika Uchumi wa Buluu lililofanyika sambamba na Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika Dar es Salaam kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026.

Kongamano hilo lenye kaulimbiu “Kufungua Fursa za Uwekezaji, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu wa Buluu”, limewakutanisha viongozi wa Serikali, wawekezaji, taasisi za fedha, watafiti, wajasiriamali na washirika wa maendeleo kwa lengo la kubaini fursa za uwekezaji katika Bahari ya Hindi Magharibi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Rasilimali za Baharini Zanzibar (ZAFIRI), Dk. Zachara Hamisi, amesema uchumi wa bahari una fursa kubwa katika sekta za uvuvi, ufugaji wa viumbe vya majini, bidhaa za baharini, utalii, hewa ya kaboni ya baharini na bioteknolojia.

Amesema uchumi wa bahari duniani una thamani ya takribani Dola bilioni 2.6 na unatarajiwa kufikia Dola trilioni 3 ifikapo mwaka 2030, huku utafiti wa mwaka 2017 ukikadiria thamani ya uchumi wa Bahari ya Hindi Magharibi kufikia Dola bilioni 13.9.

“Tuko hapa leo kujadili namna tunavyoweza kuhakikisha kiasi hicho kinachozunguka kinabaki katika uchumi wa nchi zetu,” amesema Dk. Hamisi, akitoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji ili kuhakikisha sehemu kubwa ya thamani inayotokana na rasilimali za baharini inabaki katika uchumi wa ndani.

Amesema fursa mpya katika kaboni ya baharini, bioteknolojia ya baharini na matumizi endelevu ya mifumo ya ikolojia ya bahari zinaweza kuongezea shughuli za jadi kama uvuvi na ufugaji wa viumbe vya majini, lakini zinahitaji uwekezaji katika teknolojia, ubunifu na mifumo sahihi ya fedha.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Uratibu wa Uchumi wa Buluu, Mondy Muhando, amesema changamoto kubwa ni namna ya kugeuza utajiri wa rasilimali za baharini uliopo katika ukanda huo kuwa uwekezaji halisi.

“Changamoto yetu ni kugeuza tulichonacho kuwa uwekezaji,” amesema Muhando, akitoa wito wa kubadili mifumo ya jadi ya biashara na kutumia mbinu zinazounganisha teknolojia, fedha, taasisi, jamii na wajasiriamali.

Amesema mafanikio ya uwekezaji katika Uchumi wa Buluu hayapaswi kupimwa kwa kiwango cha biashara kinachozalishwa pekee, bali pia kwa kuangalia iwapo shughuli hizo zinafanyika kwa njia endelevu na zinahifadhi rasilimali za baharini kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Theuri Mwangi kutoka Sekretarieti ya Mkataba wa Nairobi na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), amesema uvuvi endelevu, ufugaji wa viumbe vya majini, kaboni ya baharini na utalii wa baharini vina fursa kubwa katika ukanda huo.

Amesema wawekezaji na Serikali wanapaswa kwanza kubaini wadau, migongano inayoweza kujitokeza na maslahi yanayokinzana, huku wakihakikisha jamii zinashirikishwa katika upangaji na utekelezaji wa miradi.

“Ni wakati sasa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika hili,” amesema Mwangi, akisisitiza kuwa mifumo ya fedha inapaswa kuzijumuisha jamii za maeneo husika ili ziweze kunufaika kiuchumi huku zikishiriki katika uhifadhi.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Maduhu Kazi, amesema kongamano hilo linalenga kuwaunganisha wawekezaji, taasisi za fedha, watafiti, wabunifu na wajasiriamali na fursa halisi katika uchumi wa baharini na maeneo ya pwani.

Amezitaja nishati jadidifu, bioteknolojia, uongezaji thamani na biashara nyingine za baharini na pwani kuwa miongoni mwa maeneo yanayoibuka kwa ajili ya uwekezaji, huku akisisitiza umuhimu wa utayari wa uwekezaji, upatikanaji wa fedha na uhakikisho dhidi ya hatari.

“Ninawaalika washiriki kubadilishana uzoefu wa vitendo na kubaini biashara na fursa za uwekezaji, pamoja na kujenga ubia,” amesema Dk. Kazi.

Amesema kipimo kikuu cha mafanikio ya kongamano hilo kinapaswa kuwa ubia utakaoundwa, miradi itakayoandaliwa, njia za upatikanaji wa fedha zitakazobainishwa na hatua za utekelezaji zitakazochukuliwa baada ya majadiliano hayo.

spot_img

Latest articles

KABUDI: VYAMA VYA SIASA VIENDELEE KUJENGA UTAMADUNI WA MAZUNGUMZO

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu,...

MWABUKUSI ATAKA BARAZA LA VYAMA KUWA NA KAMATI YA MAKOSA YA KISIASA

Na Tatu Mohamed RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amelishauri Baraza...

BODI YA UTALII TANZANIA YATUMIA AFCON KUTANGAZA NCHI KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu TANZANIA inaendelea kutumia fursa ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika...

MPANGO WA UUNGANISHAJI UMEME KUCHOCHEA MAENDELEO YA KIUCHUMI NA KIJAMII KWA WANANCHI – MHE. NDEJEMBI

📌Ashuhudia utiaji Saini na Uzinduzi wa mpango wa ufadhili uunganishaji umeme kwa wananchi kati...

More like this

KABUDI: VYAMA VYA SIASA VIENDELEE KUJENGA UTAMADUNI WA MAZUNGUMZO

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu,...

MWABUKUSI ATAKA BARAZA LA VYAMA KUWA NA KAMATI YA MAKOSA YA KISIASA

Na Tatu Mohamed RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amelishauri Baraza...

BODI YA UTALII TANZANIA YATUMIA AFCON KUTANGAZA NCHI KIMATAIFA

Na Mwandishi Wetu TANZANIA inaendelea kutumia fursa ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika...