Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma kuhamasisha wakulima na wafugaji kutumia bima ya kilimo ili kujikinga na hasara zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali yanayoathiri uzalishaji.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TIRA, Anna Massao, amesema mamlaka hiyo imeweka kipaumbele katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, hususan bima ya kilimo, ili kuongeza uelewa na matumizi ya huduma hizo nchini.

Amesema banda la TIRA limeandaliwa mahsusi kuwapa wananchi fursa ya kupata elimu kuhusu aina mbalimbali za bima, majukumu ya mamlaka hiyo pamoja na haki zao wanapotumia huduma za bima.
“Tunawakaribisha wananchi wa Dodoma na Watanzania wote kutembelea banda letu. Hapa watapata elimu kuhusu bima ya kilimo na huduma nyingine za bima, lakini pia watafahamu majukumu ya TIRA katika kusimamia sekta ya bima nchini,” amesema Massau.
Ameeleza kuwa pamoja na kutoa elimu, TIRA ina jukumu la kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima, kuandaa kanuni na miongozo ya sekta hiyo, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za bima zenye ubora na zinazozingatia sheria.

Massau amesema maonesho hayo pia ni jukwaa la kusikiliza na kupokea malalamiko ya wananchi yanayohusu huduma za bima, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na kuongeza imani ya wananchi katika sekta hiyo.
“Tunawasihi wananchi wenye changamoto au malalamiko yanayohusu huduma za bima wafike katika banda letu. Maafisa wetu wapo tayari kusikiliza, kutoa ushauri na kuelekeza namna ya kutatua changamoto hizo,” amesema.
Ameongeza kuwa katika banda la TIRA pia wapo wadau mbalimbali wa sekta ya bima, wakiwemo kampuni za bima, wawakilishi wa sekta kutoka Zanzibar pamoja na Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima, ambao wanatoa huduma na elimu kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo.
Kwa mujibu wa TIRA, ushiriki wake katika maonesho ya Nanenane ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu bima, kuimarisha matumizi ya huduma za bima na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia kinga dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha hasara kwa wakulima na wafugaji.
Mwisho


