Na Mwandishi Wetu
UMOJA wa Makampuni ya Bima za Kilimo Tanzania (TAIC) umewahimiza wakulima na wafugaji nchini kutumia huduma za bima ili kulinda mitaji yao dhidi ya majanga yanayoweza kusababisha hasara na kuvuruga uzalishaji.
Wito huo umetolewa katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo wadau wa sekta ya bima walisema matumizi ya bima ni nyenzo muhimu ya kuongeza uhakika wa uwekezaji katika kilimo na ufugaji, sekta zinazobeba uchumi wa wananchi wengi nchini.
Akizungumza katika banda la TAIC, mwakilishi wa Kampuni ya Bim ya Heritage, Bartazari Ndomba, amesema bima za kilimo na mifugo zimebuniwa kumlinda mkulima na mfugaji dhidi ya athari za majanga mbalimbali, yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, mvua za mawe, magonjwa ya mifugo na mazao pamoja na vihatarishi vingine vinavyotambuliwa kwenye mkataba wa bima.

Amesema mkulima anapopata hasara kutokana na janga lililokatiwa bima hulipwa fidia, hatua inayomwezesha kurejesha sehemu ya mtaji wake na kuendelea na uzalishaji bila kuanza upya.
“Bima inalinda uwekezaji wa mkulima na mfugaji. Badala ya kupoteza kila kitu baada ya janga, anapata fidia inayomwezesha kuendelea na shughuli zake za uzalishaji,” amesema.
Ndomba ameongeza kuwa huduma hizo zinapatikana kwa makundi mbalimbali ya wazalishaji, wakiwemo wakulima wa mazao, wafugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na hata wafugaji wa samaki, huku gharama ya bima ikitegemea aina ya shughuli na thamani ya mali inayohifadhiwa.
Kwa upande wake, Afisa Biashara Kampuni ya Bima Mtawanyo, Agustino Ndabaha, amesema makampuni ya bima mtawanyo yana jukumu la kuongeza uwezo wa kifedha wa makampuni yanayotoa bima za kilimo ili yaweze kuwafikia wakulima wengi zaidi na kuwa na uwezo wa kulipa madai makubwa pale majanga yanapotokea.

Amesema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo kwa maisha yao, hivyo ni muhimu kuhakikisha sekta hiyo inalindwa kwa mifumo imara ya bima.
“Kazi yetu ni kuongeza nguvu za kifedha kwa makampuni ya bima ili yaweze kuandikisha wakulima wengi zaidi na kulipa madai kwa wakati pale majanga yanapotokea. Hii inaongeza imani kwa wakulima na kuimarisha sekta ya kilimo,” amesema Ndabaha.
Ameongeza kuwa kaulimbiu ya Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu inahimiza wakulima na wafugaji kulinda mazao na mifugo yao ili kuongeza tija na uzalishaji, akisema matumizi ya bima ni sehemu muhimu ya kufanikisha lengo hilo.

Ndabaha amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea banda la TAIC ili kupata elimu kuhusu aina mbalimbali za bima za kilimo, haki na wajibu wa wanunuzi wa bima pamoja na namna ya kupata fidia endapo majanga yatatokea.
Naye Busiga Massaka kutoka Tanzania Reinsuarance Company Limited (TAN-RE) amesema makampuni ya bima mtawanyo yanaendelea kuimarisha uwezo wa kifedha wa makampuni yanayowahudumia wakulima na wafugaji ili kuhakikisha yanatoa huduma kwa wigo mpana zaidi.
Amesema banda la TAIC limewakutanisha pamoja watoa huduma mbalimbali wa bima za kilimo na mifugo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda uwekezaji wao.
“Tunawahimiza wakulima na wafugaji kuchukua bima za mazao na mifugo kupitia Tanzania Agriculture Insurance Company (TAIC), ambao ni muunganiko wa makampuni ya bima yanayoshirikiana kutoa huduma hizi. Kupitia banda hili wananchi wanapata elimu ya kina kuhusu namna bima inavyoweza kuwalinda dhidi ya hasara zinazotokana na majanga,” amesema Massaka.
Wadau hao wamesema matumizi ya bima yanaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga kilimo chenye tija na chenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku yakiwapa wakulima na wafugaji uhakika wa kuendelea na uzalishaji hata baada ya kukumbwa na majanga.


