Na Mwandishi Wetu
KAIMU Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bwn. Natalis Linuma, amesema Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) ni mdau muhimu katika kuhakikisha matumizi ya mionzi yanafanyika kwa usalama katika sekta mbalimbali, ikiwemo hospitali, viwanda, vituo vya utafiti, migodi, bandari, viwanja vya ndege pamoja na miradi ya ujenzi wa barabara na reli.
Linuma ameyasema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wataalamu wa TAEC waliofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi kujitambulisha kabla ya kuanza ukaguzi wa vituo vinavyotumia vyanzo vya mionzi mkoani humo.

“Karibuni katika Mkoa wa Lindi. TAEC ni mdau muhimu katika kuhakikisha matumizi ya mionzi yanafanyika kwa usalama. Ujio wenu ni chachu katika kuhakikisha Mkoa wa Lindi unaendelea kuwa salama katika matumizi ya mionzi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi,” amesema Linuma.
Kwa upande wake, Afisa Mkaguzi Mwandamizi wa Mionzi wa TAEC, Bwn. Mungubariki Nyaki, amesema Tume inafanya ukaguzi katika vituo 32 mkoani Lindi kwa lengo la kujiridhisha kuwa watumiaji wa vyanzo vya mionzi wanazingatia sheria, taratibu na kanuni za usalama wa mionzi.

Amesema ukaguzi huo pia unalenga kuwakumbusha wamiliki na watumiaji wa vyanzo vya mionzi kuhakikisha wanakuwa na leseni halali za umiliki na matumizi ya vyanzo hivyo, pamoja na kutekeleza masharti yote ya usalama yanayotakiwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine, Dkt. Alexander Makalla, ameishukuru TAEC kwa ushirikiano na ushauri wa kitaalamu inaoutoa kwa hospitali hiyo, hususan wakati wa ujenzi wa majengo yanayohifadhi mashine zinazotumia mionzi na katika kuwawezesha watendaji kuzingatia matakwa ya usalama wanapotekeleza majukumu yao.

Amesema ushirikiano huo umeendelea kuwa muhimu katika mipango ya hospitali ya kuboresha huduma zake, ikiwemo huduma za kinywa na meno.
“Kwa mfano, sasa tunatarajia kuimarisha huduma za kinywa na meno. Tuliwasiliana na wataalamu wa TAEC kabla ya kuagiza mashine ya kisasa kwa ajili ya huduma hizo. Kwa ujumla TAEC wanatusaidia sana, na wanapobaini mapungufu wakati wa ukaguzi hutupatia ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kuyarekebisha,” amesema Dkt. Makalla.

Ukaguzi huo ni sehemu ya majukumu ya TAEC ya kuhakikisha matumizi ya vyanzo vya mionzi nchini yanafanyika kwa kuzingatia matakwa ya usalama ili kuwalinda wagonjwa, wafanyakazi, wananchi na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kutokana na matumizi yasiyo salama ya mionzi.


