Wakulima wahimizwa kudai haki zao za bima kupitia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima

Na Mwandishi Wetu

WAKULIMA nchini wamehimizwa kufahamu haki zao wanapokata bima ya mazao kupitia benki au mawakala wa bima kwa kutumia Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO) kutatua migogoro ya fidia kwa haraka badala ya kukimbilia mahakamani.

Wito huo umetolewa na Msuluhishi Mkuu wa Migogoro ya Bima, Aloyce Mbunito, wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo amesema ofisi hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima, Sura ya 394, ili kutoa suluhisho la haraka, nafuu na lenye haki kwa wananchi wanaokumbana na migogoro ya bima.

Mbunito amesema pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika sekta ya bima, ofisi hiyo inapokea na kushughulikia migogoro mbalimbali inayotokana na huduma za bima, ikiwemo madai ya fidia kukataliwa, kucheleweshwa, kulipwa kiwango kisicholingana na hasara halisi au kutokuelewana kuhusu masharti ya mikataba ya bima.

Amesema tangu kuanza kwa shughuli za ofisi hiyo mwaka 2025, zaidi ya migogoro 2,015 imetatuliwa, hatua ambayo imeongeza imani ya wananchi katika matumizi ya mifumo ya usuluhishi wa migogoro nje ya mahakama.

“Matokeo haya yanaonyesha kuwa wananchi wameanza kutambua kuwa wana sehemu salama ya kudai haki zao wanapokumbana na changamoto katika huduma za bima,” alisema Mbunito.

Amebainisha kuwa wakati wa maonesho hayo viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima kutoka mkoani Mara walifika katika banda la ofisi hiyo kuwasilisha changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku waliopata hasara kutokana na mvua ya mawe, licha ya kuwa walikuwa wamekata bima kupitia benki.

Kwa mujibu wa Mbunito, uchunguzi wa awali umebaini kuwa wakulima wengi hawakujua kampuni za bima zilizowahudumia kwa sababu walikata bima kupitia benki zilizokuwa zikifanya kazi kama mawakala wa bima huku wengi hawakuwa na nakala za mikataba ya bima, hali iliyochangia ugumu katika kufuatilia madai yao ya fidia.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wakulima kuhakikisha wanapata na kuhifadhi mikataba ya bima pamoja na nyaraka nyingine muhimu kila wanaponunua huduma za bima ili kurahisisha mchakato wa kudai fidia pindi majanga yanapotokea.

Naye Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mara (WAMACU), Momanyi Range, amesema elimu waliyoipata katika banda la Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima imewapa uelewa mpya kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mikataba ya bima na vielelezo vinavyothibitisha hasara, ikiwemo picha za mazao yaliyoharibiwa.

Range amesema chama hicho kimeanza kuratibu ukusanyaji wa malalamiko ya wakulima walioathirika, kuwasaidia kupata mikataba yao kutoka benki husika na kuwasilisha mashauri yao katika Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima ili kuhakikisha wanapata fidia stahiki na kurejea katika shughuli za uzalishaji bila kuendelea kubeba athari za hasara zilizowakumba.

Mwisho

spot_img

Latest articles

UKAGUZI WA MIGODI WAIMARISHA USALAMA, UHIFADHI WA MAZINGIRA

Tume ya Madini yasisitiza uchimbaji unaozingatia sheria, afya na maendeleo endelevu Na Mwandishi Wetu...

Mhitimu wa VETA abuni mashine ya kupunguza gharama za ufugaji na kuongeza thamani ya mazao

Na Mwandishi Wetu MHITIMU wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, Ernest Maranya, amebuni mashine...

WMA YAWAFUNDISHA WATOTO VIPIMO: NAIBU WAZIRI MALIASILI APONGEZA

Na Mwandishi Wetu NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amefurahishwa na...

GST: Taarifa sahihi za kijiolojia ni msingi wa uchimbaji wenye tija

Na Mwandishi Wetu TAASISI ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewataka wachimbaji,...

More like this

UKAGUZI WA MIGODI WAIMARISHA USALAMA, UHIFADHI WA MAZINGIRA

Tume ya Madini yasisitiza uchimbaji unaozingatia sheria, afya na maendeleo endelevu Na Mwandishi Wetu...

Mhitimu wa VETA abuni mashine ya kupunguza gharama za ufugaji na kuongeza thamani ya mazao

Na Mwandishi Wetu MHITIMU wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, Ernest Maranya, amebuni mashine...

WMA YAWAFUNDISHA WATOTO VIPIMO: NAIBU WAZIRI MALIASILI APONGEZA

Na Mwandishi Wetu NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, amefurahishwa na...