Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imepokea mhamasishaji amani duniani, Saddam Alaya (Mr. Alaya), ambaye anatekeleza safari ya kihistoria ya The World’s Longest Peace Walk, inayolenga kuweka rekodi ya Guinness World Records kupitia matembezi marefu zaidi ya kuhamasisha amani duniani.

Alaya ameingia nchini Agosti 2,2026 kupitia Mpaka wa Kasesya uliopo Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa, na kuanza rasmi safari ya takribani siku 35 ndani ya Tanzania.
Katika kipindi hicho atatembea kupitia mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma kabla ya kuondoka nchini kupitia Mpaka wa Manyovu.Mapokezi hayo yameratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Tanzania Safari Channel.

Imeelezwa kuwa lengo la safari hiyo ni kuhamasisha amani, mshikamano wa kimataifa na urafiki miongoni mwa mataifa, sambamba na kuitangaza Tanzania kama moja ya vivutio vinavyoongoza vya utalii duniani.
Safari ya Mr. Alaya ni sehemu ya mradi wa kimataifa unaolenga kutembea zaidi ya kilomita 23,000 kutoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Magadan, Urusi, kupitia nchi 18 kuanzia mwaka 2026 hadi 2028.

Tanzania imekuwa nchi ya tano katika ratiba ya safari hiyo, hatua inayotoa fursa ya kipekee ya kuonesha vivutio vya utalii, urithi wa asili, utamaduni na ukarimu wa Watanzania kwa hadhira ya kimataifa.
Mbali na kuhamasisha amani, safari hiyo pia inalenga kuweka rekodi saba za Guinness World Records, jambo linalotarajiwa kuongeza mvuto wa mradi huo katika jukwaa la kimataifa.

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TTB inaendelea kutumia majukwaa ya kimataifa kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii, amani na urithi wa dunia, huku ikiendelea kuwakaribisha watalii na wageni kutoka kila pembe ya dunia kufika nchini na kujionea vivutio vya kipekee vilivyopo Tanzania.


