Na Mwandishi Wetu
ASKARI na mahabusu wanadaiwa kufariki dunia baada ya gari la Polisi walilokuwa wakisafiria kugongwa na lori la mizigo katika eneo la Mlima Sekenke, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 2:00 asubuhi, huku taarifa za awali zikieleza kuwa watu 12 wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, akisema taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na vikosi vya uokoaji, gari hilo la Polisi lilikuwa limebeba watu 13, wakiwamo mahabusu wanane na askari watano.
Watu hao walikuwa wakisafirisha mahabusu kutoka Kituo cha Polisi Shelui kwenda Mahakama ya Wilaya ya Iramba iliyopo Kiomboi.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya lori la mizigo lililokuwa likisafirisha mafuta ya dizeli kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Rwanda kufeli breki wakati likishuka katika eneo la Mlima Sekenke.
Lori hilo linadaiwa kuligonga gari hilo la Polisi, na kusababisha ajali hiyo.
Baada ya ajali, majeruhi waliokolewa na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo, taarifa zaidi kuhusu idadi kamili ya waliopoteza maisha, majeruhi pamoja na chanzo rasmi cha ajali hiyo zinatarajiwa kutolewa na mamlaka husika.


