Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia vifo vya watu 12, wakiwemo mahabusu saba na askari polisi watano, vilivyotokea leo katika Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, baada ya ajali iliyohusisha gari la Jeshi la Polisi na lori.
Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Omary Dendego, familia za marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania wote kufuatia msiba huo.
Aidha, amewasisitiza madereva wote kuzingatia Sheria za Usalama Barabarani na kuhakikisha vyombo vya moto vinakuwa katika hali nzuri na salama kabla ya kutumika, ili kulinda maisha ya wananchi na watumiaji wengine wa barabara.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida, ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Singida–Nzega eneo la Mlima Sekenke, ilihusisha lori lenye namba za usajili RAF 243X/TRL 4255, mali ya Kampuni ya YYUSSA ya Kigali, Rwanda na gari la Jeshi la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser PT 1982.
Polisi imesema lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Ndanarasa Christian Alfonce, raia wa Rwanda, lilikuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Rwanda, wakati gari la Polisi lililokuwa likiendeshwa na Staff Sajenti (S/SGT) Ussi Hassan likitokea Kituo cha Polisi Shelui kuelekea Kiomboi kuwapeleka Watuhumiwa mahakamani.
Waliofariki katika ajali hiyo ni Askari watano wa Jeshi la Polisi ambao ni SP Frank Lazima Mwasapili, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Shelui, S/SGT Ussi Hassan, SGT Paulo Silvin Gabriel, PC Ashraf Salumu Kheri na PC Nangida Ramadhani Mushi.
Wengine waliofariki ni Mahabusu saba ambao ni Timotheo Lazaro Kimaro, Cassian Hassan, Fred Musuguli Mzoa, Wilfred Marko Amos, Mariam Hamis Kasijao, Vivian Saidi na Hussen Hussen Kea, huku waliojeruhiwa ni Mahabusu Petro Organes Nkana na dereva wa lori Ndanarasa Christian Alfonce.


