📌 Aomba radhi kwa wateja wananchi na kuwahakikishia upatikanaji endelevu wa huduma ya umeme
📌 Asema uzalishaji wa umeme umefikia megawati 4400 na juhudi za kuimarisha Mfumo wa Gridi zinaendelea
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, leo amewaomba radhi wananchi na wateja wote wa huduma ya umeme kufuatia hitilafu iliyojitokeza kwenye Mfumo wa Gridi ya Umeme ya Taifa siku ya jana Juni 27, 2026, iliyosababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 28, 2026, Bw. Twange amesema uchunguzi wa awali uliofanywa wakati wa hatua za kurejesha huduma umebaini kuwa kutoka kwa Gridi kulisababishwa na hitilafu zilizojitokeza kwa wakati mmoja katika njia tatu za usafirishaji wa umeme pamoja na mashine moja ya kuzalisha umeme.

Ameeleza kuwa , Gridi ya Umeme ya Taifa ni mfumo mmoja unaounganisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, hivyo hitilafu kubwa inapotokea katika sehemu mojawapo ya mfumo huo inaweza kuathiri utendaji wa Gridi nzima na kusababisha kukosekana kwa huduma ya umeme katika maeneo mengi kwa wakati mmoja.
“Tunatambua usumbufu uliowakumba wananchi na wateja wetu kutokana na hitilafu hii, na tunawaomba radhi. Wataalamu wetu walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa haraka na kwa usalama,”amesema Bw. Twange.

Pamoja na hayo , amesema licha ya uwepo wa tukio hilo, hali ya uzalishaji wa umeme nchini inaendelea kuwa imara, ambapo uwezo wa uzalishaji umefikia takribani megawati 4,400 kiwango ambacho kinatosheleza mahitaji ya sasa ya nchi.
“Tunawaomba wananchi waendelee kuwa na imani na TANESCO. Sambamba na kuendelea kuimarisha uzalishaji wa umeme, tunawekeza katika kuboresha miundombinu ya Gridi ya Taifa ili kuongeza uthabiti wa mfumo na kupunguza uwezekano wa kujitokeza kwa hitilafu za aina za aina hii siku za usoni. Dhamira yetu ni kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme ya uhakika, salama na endelevu,”ameongeza Bw. Twange.
Aidha, amesema TANESCO inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha uthabiti wa Mfumo wa Gridi ya Taifa kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, hatua inayolenga kupunguza uwezekano wa kujirudia kwa hitilafu za aina hiyo na kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii haziathiriki.

Amewahakikishia wananchi kuwa TANESCO itaendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme, huku ikiendeleza juhudi za kuimarisha mawasiliano na mahusiano bora na wateja ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma nchini.
Katika hatua nyingine, amesisitiza kuwa, Shirika litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuimarisha mifumo ya umeme nchini ili wananchi waendelee kupata huduma ya uhakika, salama na endelevu.


