Hatuna pa kujificha, tuwajibike tu yaishe

TAIFA la Tanzania ni nchi huru iliyojitawala kwa takribani miaka 65 sasa, tangu bendera ya Muingereza iliposhushwa Desemba 9, 1961. Taifa hili pia ni sehemu ya jumuiya ya kimataifa. Ndiyo maana tangu uhuru, Tanzania imekuwa ikisumbuka kwa kujihusisha na mambo mengi ya jumuiya ya kimataifa.

Ni katika muktadha huo, siyo tu kwamba Tanzania imekuwa mshirika katika harakati za jumuiya ya kimatifa, bali inatajwa kuwa kitovu cha mapambano ya kudai haki. Kusukuma harakati za kutokomeza ukoloni katika bara la Afrika. Tanzania imetumia rasilimali zake nyingi kwa ajili ya kutetea wanyonge kokote katika dunia hii. Tanzania kihistoria imejipambanua kama kimbilio la wote wanaoonewa na kupuuzwa. Tanzania kwa miaka na miaka ilitoa ardhi ya watu wake, chakula cha watu wake, na hata damu za watu wake kwa ajili ya kupigania haki. Kwa ajili ya kutokomeza uonevu na dhuluma. Kwa ajili ya ukombozi wa wote wanaonewa.

Haya ndiyo yamekuwa utambulisho wa Taifa linaloitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Utambulisho huu ni fahari. Hata maandiko matakatifu, iwe ni Biblia au Kurani tukufu, yanatambua kuwa sifa mojawapo ya Mungu ni haki. Kuwatetea na kuwasitiri wanaoonewa, kuwapigania wanyonge na kuwapa tumaini. Hii ni sifa uungu.

Kwa mantiki hiyo, Tanzania inaweza kutajwa kama taifa ambalo lilikuwa linatekeleza sifa ya uungu. Kutetea wanyonge, kuwapa tumaini na kuwalisha kila ilipobidi. Kuwatafutia haki.

Sifa hii murua ya taifa letu ndiyo ilitutambulisha. Na kila tulipojadiliwa huku duniani na mataifa makubwa, yalitujadili kwa sura hiyo. Taifa lenye msimamo juu ya haki za watu. Juu ya kuondoa ukandamizaji, unyonge na kuheshimu haki za kila binadamu bila kujali rangi.

Ndiyo maana tangu awali mara tu baada ya uhuru, taifa hili lijengwa kwenye msingi wa haki ya kweli iliyojumuisha usawa wa watu, utu wa binadamu, ushiriki wa wananchi katika uongozi, na haki ya kiuchumi pamoja na haki za kiraia.

Kokote kwenye majukwaa ya kisiasa ya kimataifa Tanzania ilipotajwa ilijadiliwa kama mshirika wa kutetea haki, mdau wa jumuiya ya kimataifa wa kuondosha unyonge, ukandamizaji na dhuluma za aina zote dhidi ya binadamu.

Wakati wahenga wakiendelea kutafakari juu ya haiba ya Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyojengwa kwa kitambo chote hicho, wanajawa na majonzi kila wanaposikia kwa sasa taifa hili likitajwa huku duniani ni kwenye shutuma. Linashutumiwa kwa mengi.

Mwanzoni mwa mwezi huu, yaani Juni 3, 2026, katika Bunge la Ulaya, Kamati ya Mambo ya Nje  na Kamati ya Maendeleo zilipiga kura kupinga uamuzi wa Tume ya Ulaya wa kutoa euro milioni 156 (Tsh466.86bn) kwa Mpango wa Maendeleo wa Tanzania wa mwaka 2026 (Annual Action Plan for Tanzania 2026). Uamuzi huo ulipita kwa kura 81 za kuunga mkono pingamizi hilo, wakati kura moja ilipinga, aidha, kura nne kutopiga upande wowote.

Kwa lugha rahisi, wabunge hao walikuwa wakisema hawakubaliani na Tume ya Ulaya kuendelea na mpango wa kuifadhili Tanzania bila kwanza kushughulikia wasiwasi ulioelezwa kuhusu uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025, masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na mazingira ya kisiasa yaliyopo nchini.

Hivyo basi, waliitaka Tume ya Ulaya kuondoa au kurekebisha mpango huo wa ufadhili kwa kuzingatia wasiwasi wao ambao kwa kitambo umekuwa ni hoja inayofungamanishwa na ufadhili huo.

Nini kinaweza kutokea juu ya kura hii sasa? Moja ni uwezekano wa kucheleweshwa au kuzuiwa sehemu ya fedha za maendeleo kutoka EU; na kuongezeka kwa shinikizo la kidiplomasia kwa Tanzania. Hata hivyo, kura hiyo haiathiri moja kwa moja biashara wala uanachama wa Tanzania katika jumuiya za kimataifa.

Kwa hakika, hizi siyo fedha nyingi ambazo zinaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa sehemu kubwa. Fedha hizi Tanzania inaweza kuzipata kwa vyanzo vyake vya ndani. Inawezekana kabisa.

Hata hivyo, hoja hapa siyo wingi au uchache wa fedha. Suala hapa ni hadhi ya Taifa. Suala hapa ni tuhuma tunazobeba. Kwa miaka na miaka Tanzania haikuwa nchi ya kutajwa kwenye masuala ya ukiukaji wa haki za wananchi wake, uchaguzi uliojaa figisufigisu, ukanyagaji wa haki za kisiasa za wananchi wake, kiasi cha kuibua kilio cha jumuiya ya kimataifa dhidi yetu.

Kwamba sasa ni kama Tanzania imebadili sura kutoka taifa kinara wa kutetea haki za wanyonge na kupinga uonevu kama ambavyo ilifanya katika harakati za ukombozi wa Afrika- hususani Kusini mwa Afrika, kutetea haki za Wapalestina na hata haki za Polisario – Sahara Magharibi, na sasa inakuwa taifa linalokandamiza na kukalia haki za raia wake. Kuvunja misingi ya demokrasia na kuratibu vitendo vya utekaji na mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.

Kuna watu wanaoweza kudhani kwamba haya yanayotokea huku kwenye jumuiya ya kimataifa hayana maana, hayatutishi, tunaweza kuendelea na kutekeleza majukumu yetu bila wao. Haya yanaweza kuwa ni aina ya mawazo yanayosukumwa kwenye safu za uongozi kiasi cha kuwalisha viongozi fikra hizo. Kwa bahati mbaya, hizi fikra zinaweza kumezwa na kuwa ndiyo simulizi pendwa (a loved narrative). Hii ni hatari kubwa!

Ni bahati mbaya kwamba viwango vya weledi katika kutafuta watu wafaao kukalia ofisi za umma vimeshuka mno kiasi kwamba hata haya yanayotokea dhidi ya taifa huko Ulaya na hata yanayoendelea kuchemka kwenye Bunge la Marekani, haionekani kuwa ni kitu cha kuwashitua.

Nimesema hapo awali, kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi huru, pamoja na uhuru huo, ni sehemu ya jumuiya ya kimataifa. Kwa sura na msukumo ule ule tulioona kwamba walowezi wa wachache wa Zimbabwe hawakuwatendea haki walio wengi nchini kule, au kwa msimamo ule ule tulioona Makaburu wa Afrika Kusini hawakuwa na haki ya kuwatendea uovu weusi walio wengi katika nchi ile, hivyo kutaka nchi hizi ziwe huru na kila raia apate haki yake; ni kiwango kile kile jumuiya ya kimataifa inatupima. Kwamba pamoja na uhuru wetu, je, haki za raia zinalindwa? Je, misingi ya demokrasia ikiwa ni pamoja na haki ya wananchi kujichagulia viongozi wanaowataka inalindwa na kuheshimiwa? Na je, uwajibikaji uliosawa mbele ya sheria bila ubaguzi na kuoneana vinaenziwa? Tukiwa sehemu ya jumuiya ya kimataifa, hatuna pa kujificha, ni lazima tujiweke kwenye mzani ili tupimwe kwenye haya mambo ambayo kama taifa tuliyaridhia na kukubali kuyafuata. Hakuna pa kujificha.

spot_img

Latest articles

MD TWANGE ATOA RAI KWA MAMENEJA TANESCO KUONGEZA KASI YA KUPAMBANA NA WIZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

📌Afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, Dodoma 📌Asisitiza umuhimu wa...

Yanga yakomaa kileleni, Simba yavizia ikitafuna  miwa Morogoro

Na Mwandishi Wetu WANANCHI Yanga wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu...

WIZARA YA NISHATI YAENDELEA KUTUMIA NISHATI SAFI EXPO KUTOA ELIMU KWA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Nishati inaendelea kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia...

Wiki ya Utumishi wa Umma yasogeza huduma za Taasisi za Umma karibu na wananchi

Na Mwandishi Wetu Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2026 yameonesha...

More like this

MD TWANGE ATOA RAI KWA MAMENEJA TANESCO KUONGEZA KASI YA KUPAMBANA NA WIZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME

📌Afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, Dodoma 📌Asisitiza umuhimu wa...

Yanga yakomaa kileleni, Simba yavizia ikitafuna  miwa Morogoro

Na Mwandishi Wetu WANANCHI Yanga wamejiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu...

WIZARA YA NISHATI YAENDELEA KUTUMIA NISHATI SAFI EXPO KUTOA ELIMU KWA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Nishati inaendelea kutoa elimu ya nishati safi ya kupikia...