Na Mwandishi Wetu, Dodoma
JESHI la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatua za kuchukua wakati wa majanga, likiwataka kujifunza mbinu sahihi za uokoaji na matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na uokozi ili kupunguza madhara na kuokoa maisha.
Elimu hiyo imetolewa katika Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, ambapo wananchi wamepewa mafunzo kuhusu namna ya kukabiliana na majanga katika hatua za awali kabla ya kufika kwa vikosi vya uokoaji.

Jeshi hilo limeeleza kuwa uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kuchukua hatua sahihi wakati wa majanga ni muhimu, kwa kuwa hatua zinazochukuliwa katika dakika za mwanzo zinaweza kusaidia kuzuia madhara zaidi na kuokoa maisha.
Aidha, wananchi wamefundishwa namna ya kutumia vifaa mbalimbali vya uokoaji kwa usahihi, huku wakisisitizwa kutochukua hatua zinazoweza kuongeza hatari kwao au kwa watu wengine wakati wa kutoa msaada.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pia limewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kutoa taarifa kwa haraka pindi janga linapotokea, ili kuwezesha vikosi vya uokoaji kufika eneo la tukio kwa wakati na kutoa msaada unaohitajika.
Limesema ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa kwa wakati na kufuata maelekezo ya wataalamu ni sehemu muhimu ya kupunguza madhara yanayosababishwa na majanga.

Kupitia Maonesho ya Nanenane, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeendelea kutumia fursa hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwajengea uelewa kuhusu kinga dhidi ya majanga, hatua za awali za uokoaji na matumizi salama ya vifaa vya kukabiliana na moto na majanga mengine.



