Na Mwandishi Wetu
OFISI ya Msajili wa Hazina imetangaza siku ya Gawio 2026 itafanyika Juni 30, 2026 katika Ikulu ya Dar es Salaam, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Tukio hilo limeelezwa kuwa la kihistoria katika usimamizi wa mali na uwekezaji wa Serikali kwa kuwa linatoa fursa ya kuonesha matokeo ya uwekezaji wa umma kwa wananchi.
Kupitia hafla hiyo, taasisi za umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa zitawasilisha gawio pamoja na michango mingine kwa Serikali.

Mapato hayo yanatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kugharamia miradi ya maendeleo inayogusa sekta muhimu zikiwemo elimu, afya, maji, nishati na miundombinu.
Kauli mbiu ya Siku ya Gawio 2026 ni “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu Kuelekea Dira 2050”. Serikali imeeleza kuwa kauli mbiu hiyo inalenga kuhimiza matumizi yenye tija ya rasilimali za umma ili kuhakikisha uwekezaji unaofanywa kwa niaba ya wananchi unazalisha matokeo yanayoonekana na kupimika.
Akiongea na waandishi wa habari, Jumatatu, Juni 16, 2026, Bi. Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara, amesema uwekezaji wa umma ukisimamiwa kwa weledi, uwajibikaji na ufanisi unakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Aidha, taasisi za umma zina nafasi muhimu katika kusaidia utekelezaji wa Dira 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na endelevu.
Siku ya Gawio imeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kuonesha matokeo ya uwekezaji wa Serikali, kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya mali za umma pamoja na kuthibitisha mchango wa mashirika na taasisi za umma katika maendeleo ya taifa.
Ofisi ya Msajili wa Hazina pia imezipongeza taasisi na kampuni ambazo tayari zimewasilisha gawio na michango yao kwa wakati, ikieleza kuwa hatua hiyo inaonesha kiwango cha juu cha uwajibikaji na weledi.
Wakati huo huo, taasisi ambazo bado zinakamilisha mchakato huo zimetakiwa kutimiza wajibu wao kwa wakati ili kuhakikisha maandalizi ya tukio hilo yanafanikiwa.
Katika hafla hiyo, taasisi zitakazofanya vizuri zaidi katika utendaji na utoaji wa gawio zitatunukiwa tuzo na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Serikali inaamini kuwa utambuzi huo utahamasisha ushindani chanya, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha utamaduni wa utendaji unaozingatia matokeo katika usimamizi wa uwekezaji wa umma.
Hadi kufikia Juni 2025, Serikali ilikuwa imewekeza Sh92 trilioni katika taasisi na mashirika ya umma.
Wananchi wamehimizwa kufuatilia taarifa zitakazotolewa kabla, wakati na baada ya Siku ya Gawio 2026 ili kujionea matokeo ya uwekezaji huo na mchango wake katika kujenga uchumi shindani na maendeleo endelevu kuelekea Dira 2050.


