Tunazidi kujisokota kwenye mtego, au tunajinasua?

TAIFA limechafukwa. Kuchafukwa huku ni kutokana na kile ambacho maseneta wawili wa Marekani, Jeanne Shaheen na Ted Cruz wameandaa. Hiki ni muswada unaoitwa Reassessing the United States–Tanzania Bilateral Relationship Act kwa Kiswahili kisicho rasmi ni Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Uhusiano wa Kimataifa wa Pande Mbili kati ya Marekani na Tanzania. Muswada huu uliwasilishwa kwenye bunge la Marekani Mei 2026.

Muswada huo bado haujawa sheria, uko katika hatua za awali za mchakato wa kutunga sheria. Muswada huu kimsingi unawalenga baadhi ya viongozi wa Tanzania. Hautaji majina ya viongozi maalumu kwa sasa. Unaiagiza serikali ya Marekani kuandaa ripoti itakayobainisha maafisa wa serikali, chama tawala na vyombo vya usalama watakaobainika kuhusika na vurugu za kisiasa; ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu; utekaji au upotevu wa watu; ukandamizaji wa kisiasa; na vitendo vingine vinavyohusishwa na uchaguzi mkuu wa 2025.

Ingawa muswada haujawa sheria bado, baada ya mchakato wa utungwaji wa sheria kufika mwisho watu watakaotajwa wanaweza kuwekewa: marufuku ya viza vya kuingia Marekani; kuzuiwa mali au maslahi waliyonayo ndani ya mamlaka ya Marekani; na kuwekewa vikwazo vingine vya kifedha.

Muswada huu pia unaweza kusababisha kupitiwa upya kwa ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania katika masuala ya kiusalama, kiuchumi na kidiplomasia. Kwa maana hii, baadhi ya misaada ya maendeleo na usalama inaweza kusimamishwa hadi pale Marekani itakaporidhika kuwa kuna mageuzi ya kisiasa na haki za binadamu yamefanyika.

Hatua hizi zinaweza kuwa na athari za moja kwa moja kwa miradi inayofadhiliwa na Marekani. Aidha, kuna uwezekano wa kuathiri uwekezaji na taswira ya Tanzania mbele ya baadhi ya wawekezaji wa kimataifa endapo uhusiano wa nchi hizi mbili utazorota.

Kwa kuwa muswada huu umeungwa mkono na seneta wa chama cha Democratic na wa Republican, una uzito wa kisiasa kuliko muswada wa chama kimoja. Hata hivyo, ni lazima upitie hatua kadhaa katika Bunge la Marekani na hatimaye kutiwa saini na rais ili uwe sheria. Kwa hiyo, kwa sasa hakuna kiongozi wa Tanzania ambaye tayari amewekewa marufuku chini ya muswada huu.

Hata hivyo, pamoja na ukweli kwamba bado muswada huu haujawa sheria na madhara yake hayajaanza kutimia, umeibua taharuki kubwa. Wiki iliyopita baadhi ya wabunge waliibuka kwa hisia kali kuonyesha kuwa kusudio la muswada huo unalenga kuiumiza nchi. Aidha, wapo walioonyesha kuwa hatua ya maseneta hao inalenga kuingilia uhuru wa Tanzania kama nchi huru. Kumekuwa na vita ya maneno. Kumekuwa na kauli kali. Kuna shida.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo akiwasilisha bajeti ya wizara yake wiki iliyopita (Mei 26, 2026) alionyesha kuwa serikali imechukuwa hatua za kidiplomasia zaidi kuliko ya kushambuliana kukabili kusudio hili. Waziri Kombo alieleza kuwa ubalozi wa Washington, chini ya Balozi Elsie Kanza, umeelekezwa kushughulikia hoja zilizotolewa na maseneta wa Marekani. Aidha, alisema Tanzania tayari imewaandikia maseneta hao na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kujionea hali halisi.

Waziri pia alieleza kuwa baadhi ya madai yaliyomo kwenye muswada yanapaswa kuthibitishwa moja kwa moja badala ya kutegemea taarifa kutoka nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa Tanzania inataka kuendeleza uhusiano wake wa muda mrefu na Marekani huku ikilinda pia uhuru wake na maslahi ya taifa.

Kwa ujumla msimamo wa serikali kama ulivyoelezwa na Waziri Kombo ni kwamba muswada huo unapaswa kushughulikiwa kwa njia ya kidiplomasia na mazungumzo ya moja kwa moja badala ya kuongeza mvutano.

Hali hii inayotokea Marekani inaongeza mlango wa mapambano ya kidiplomasia katika kuonyesha kwamba bado Tanzania ni nchi inayozingatia haki za watu, hususan raia wake. Wakati serikali ikiingia katika mtanange huu, kwa muda mrefu sasa kumekuwa na taarifa zisizotiwa shaka juu ya ukiukaji wa haki za wananchi nchini.

Kumekuwako na tuhuma za watu kupotea, kutekwa na kuuawa. Taasisi za kiraia, zimeorodhesha kwa ushahidi watu waliouawa, kutekwa na kupotea katika mazingira ambayo yananyoosha kidole cha lawama kwa vyombo vya usalama nchini. Tume ya Jaji Mohamed Chande ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 imethibitisha kwamba walau watu 518 waliuawa katika matukio hayo huku wengine kwa mamia wakijeruhiwa na wengine hawajulikani waliko.

Ukiwasikiliza wabunge waliochangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wameonyesha hofu iliyochanganyika na spirit ya mapambano katika jambo linalosukumwa na maseneta wa Marekani. Wabunge wanaonyesha kwamba kuna jambo la kuzua ambalo limewasukuma watunga sheria hao wa Marekani kufikia hatua ya kuandaa muswada huo dhidi ya Tanzania.

Inawezekana wabunge hawa wanasukumwa na kile kinachoelezwa ‘msukumo wa kizalendo’ kuhusu nchi yao. Kwamba wanajiona wanao wajibu wa kutetea na kuilinda nchi yao dhidi ya uharibifu au mashambulizi dhidi ya nchi yao. Inaeleweka!

Hata hivyo, kama taifa ni kwa kiwango gani tunajiuliza swali gumu, kwamba tumefika vipi hapa? Tumefikishwa vipi hapa tulipo sasa kiasi cha kujikuta sasa taifa linaingia katika kazi ya kujitetea, kujisafisha, kutangaza upande wake. Ili hao wanaosukuma muswada wa sheria kutaka kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa serikali na chama tawala, wasitishe nia yao hiyo?

Ni hakika, hakujawahi kuwapo kwa moyo wa dhati kabisa wa kushughulikia matatizo ya mauaji, utekaji na upotezaji wa watu nchini kwa takribani miaka 10 sasa. Matukio mengi ya madhila haya dhidi ya raia siyo tu yameelezwa na ndugu wa waliouawa, kupotezwa au kutekwa, bali taasisi mbalimbali za kiraia nchini zimefanikiwa kukusanya matukio haya. Ushahidi wa madhila haya umekuwa dhahiri, lakini mamlaka ambazo zilipaswa kuchukuwa hatua kukabiliana na machungu haya ambayo jamii sasa inapitia ama zimeamua kukaa kimya au kupuuza.

Ukweli ni kwamba sisi kama taifa tumejifikisha hapa tunapoanza kuona kiwango cha kunyooshewa kidole kinaongezeka. Dunia inaona kwamba yapo mambo mengi mabaya yanafanyika nchini dhidi ya raia, lakini uharaka, msukumo na nia ya kukabili madhila dhidi ya raia haupo. Walianza Jumuiya ya Ulaya (EU) na sasa Marekani wameonyesha mwelekeo kama huo.

Jambo moja la kukumbuka ni hili, kwamba pamoja na haki ya Tanzania kama taifa huru kujiamulia mambo yake kwa uhuru, bado tunao wajibu wa pamoja kama jamii ya kimataifa kuheshimu na kulinda mikataba tulioridhia na mingine kuitungia sheria na kuwa sehemu ya katiba yetu, mojawapo kulinda haki za raia kwa gharama yoyote. Tujiulize katika eneo hilo, tunao utetezi wa kutosha ili Jumuiya ya Kimataifa isitung’ong’e?

spot_img

Latest articles

Ibenge aongezewa mkataba Azam FC

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Azam imemuongezea mkataba kocha wake, Florent Ibenge, akiendelea kusalia katika...

Mwamuzi Mtanzania kuchezesha Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu MWAMUZI wa Tanzania wa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, Shaban...

Dawasa yatoa elimu Uhifadhi wa maji katika wiki ya mazingira

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)...

Kampuni ya Media Brains yawapa mbinu za kidigitali waandishi wa habari Iringa

Na Mwandishi Wetu, Iringa KAMPUNI ya Media Brains kwa kushirikiana na Taasisi ya Konrad Adenauer...

More like this

Ibenge aongezewa mkataba Azam FC

Na Mwandishi Wetu Klabu ya Azam imemuongezea mkataba kocha wake, Florent Ibenge, akiendelea kusalia katika...

Mwamuzi Mtanzania kuchezesha Kombe la Dunia

Na Mwandishi Wetu MWAMUZI wa Tanzania wa mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu, Shaban...

Dawasa yatoa elimu Uhifadhi wa maji katika wiki ya mazingira

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)...