Waziri Ulega, RC Chalamila pekueni mafaili wizarani

KWA nyakati tofauti viongozi wawili wamezungumzia jiji la Dar es Salaam kuhusu msongamano wa magari. Msongamano wa magari kwa jiji la Dar es Salaam ni hoja muhimu ya kiuchumi, kiafya na kimazingira. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia Tanzania inapata hasara ya Sh. trilioni 1.44 kwa mwaka kutokana na foleni barabarani.

Viongozi hawa, ni Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyewaahidi wanafunzi wa uhandisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zawadi ya Sh. milioni 10 kwa atakayebuni mbinu ya kupunguza foleni Dar es Salaam. Alitoa ahadi hiyo23 Februari 2026.  Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, pamoja na mambo mengine wiki iliyopita aliibuka na mkakati wake wa kupunguza msongamano wa magari katika barabara za jiji la Dar es Salaam.

Chalamila alisema Dar es Salaam inahitaji mipango mipya ya usafirishaji na upangaji wa shughuli za uchumi. Alieleza kuwa tatizo la foleni haliwezi kutatuliwa kwa kuongeza barabara pekee, bali linahitaji mabadiliko ya kimkakati katika namna jiji linavyopangwa na kusimamiwa.

Mojawapo ya sababu kubwa za foleni alitaja kuwa ni ongezeko kubwa la magari, hasa malori yanayohusiana na shughuli za bandari; bandari kavu (dry ports) na maghala ya mizigo yaliyoenea ndani ya maeneo ya makazi; na usimamizi usio mzuri wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini. Alipendekeza kupunguza malori ndani ya jiji kwa kuelekeza nguvu kutumia bandari kavu zilizoko nje ya jiji kama Kwala; kuboresha mifumo ya bandari ili malori yasikae muda mrefu barabarani; na kuongezwa kwa ushirikiano wa taasisi zinazohusika na usafirishaji kama TANROADS, TARURA, TPA na Wakurugenzi wa halmashauri

Hata hivyo, mbali ya mamlaka hizo hapo nne, zipo nyingine nne ambazo pia hujihusisha na usafiri katika jiji la Dar es Salaam, hizi ni pamoja na Wizara ya Ujenzi inayosimamia sera na miongozo mbalimbali ya usafirishaji, DART, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, TAZARA na hata Shirika la Reli (TRC). Mamlaka zote hizi kuna mahali ama zinaingiliana au zinashirikiana katika sekta ya usafirishaji.

Viongozi hawa wawili wamegusa donda ndugu la miaka mingi katika jiji la Dar es Salaam. Katika tafiti nyingi za kitaalam ambazo zimefanywa juu ya tatizo la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam, ukiachana na kejeli za Chalamila za namba za magari yanayoanza na A kwamba ni kero; ni matatizo ya binadamu. Tatizo hili ni la kitabia.

Sababu kuu 10 za msongamano ambazo ni ongezeko kubwa la watu na magari; miundombinu dhaifu; mfumo dhaifu wa usafiri wa umma; ongezeko kubwa la malori barabarani; mipango mibovu; taa za barabarani zisizofanya kazi vizuri; ajali na magari kuharibika barabarani; ubovu wa baadhi ya barabara; maegesho finyu na kuegesha bila mpangilio uliokubalika na utitiri wa vivuko vya waenda kwa miguu na matuta barabarani.

Katika sababu zote hizi, binadamu yuko katikati ya kila sababu. Binadamu yuko katika kila sababu kwani zote zinatokana ama na maamuzi ya ovyo, au kupuuza sheria, taratibu na kanuni, vitu ambavyo vinafanaywa na binadamu.

Kwa kifupi ni kwamba tatizo kubwa la msongamano wa magari barabarani ni uamuzi wa wasimamizi wa utoaji wa leseni za vyombo vya moto bila kuvikagua juu ya umadhubuti wake wa kutumika barabarani; au maamuzi ya mihemko ya kubandika matuta na vivuko vya waenda kwa miguu barabarani ili tu kupata sifa za kisiasa; na rushwa iliyokubuhu kwa vyombo vya usimamizi wa sekta ya usafirishaji – hasa askari wa usalama barabarani.

Kwa mfano, inawezekana vipi malori mikweche kupindukia yanaruhusiwa kuwa barabarani? Au inawezekana vipi mipango iliyojaa kwenye makabrasha ndani ya Wizara ya Ujenzi haitekelezwi sawasawa na kwa wakati kwa takriani miaka 20? Inakuwaje kwa mfano mpaka leo mpango wa Dar es Salaam Transport Policy and System Development Master Plan wa mwaka 2008 tuliofadhiliwa na JAICA utekelezaji wake umekuwa ni wa chini sana. Sasa tunazungumza mpango mpya wa 2022 mpaka 2032. Lakini, ukweli ni kwamba utashi wa kuelekeza rasilimali fedha za kutosha huko uko chini sana. Hata pale pesa inapopelekwa usimamizi na uwajibikaji umekuwa ni changamoto kubwa.

Kwa mfano, nani anaweza kusema kwa yakini kabisa kwamba kwa sasa bandari kavu ya Kwala inatumika kwa kiwango cha kuridhisha ili kupunguza mzigo mkubwa wa malori yanayoingia jijini na kusababisha kero ya foleni isiyoelezeka.  Au ni nani ana ujasiri wa kuzungumzia ujenzi wa barabara za mzunguko katika jiji la Dar es Salaam, ili kuondoa ulazima wa kila gari kutumbukia katikati ya mji ili kwenda upande mwingine wa mji.

 Ninaamini Waziri Ulega pamoja na nia yake njema ya kutaka kuwaunganisha wahandisi wachanga katika mchakato wa kutafuta suluhu ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, anajua kuwa hapo Wizarani kwake kuna ripoti na taarifa nyingi za kutatua shida hii.

Miongoni mwake ni ile ya wataalamu wa usafiri na mipango miji kutoka taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, LATRA, na Benki ya Dunia ambayo walipendekeza mbinu za kupunguza foleni katika jiji la Dar es Salaam, kuwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa usafiri wa umma (mass transit); kuanzisha mfumo wa reli za mijini (commuter rail); kujenga barabara za mzunguko (ring roads);Kuondoa malori katikati ya jiji; kuweka taa za kisasa za barabarani (Smart traffic lights) hizi hutumia teknolojia kuangalia idadi ya magari na kubadilisha muda wa taa; kupanga vizuri matumizi ya ardhi (urban planning); kudhibiti maegesho ya magari (parking control) na kukuza usafiri mbadala (walking na cycling).

Rwanda nchi ambayo mwaka 1994 ilikuwa vipande vipande kutokana na mauaji ya kimbari yanayokisiwa kuua watu 800,000 na ushei, imethubutu na kufanikiwa kuondokana na mambo haya tunayohangika nayo sasa. Matumizi ya barabara nchini Rwanda ni ya nidhamu ya juu kabisa. Kila kiumbe anayeitwa binadamu ni lazima atii na kufuata sheria. Sisi hapa Tanzania ni Jamhuri ya Kambale, kila mtu ni mkubwa. Dareva bodaboda ni mkubwa, dereva bajaji ni mkubwa, mwendesha guta ni mkubwa, madereva wa daladala, magari binafsi, magari yenye namba za serikali, mashirika ya umma na magari ya majeshi kila mmoja ni mkubwa anajichukuliwa sheria mkononi.

Vurugu hizo zikichanganyika na malori mikweche yanayoharibika ovyo barabarani, kila kampuni ya mabasi kujitafutia stendi yake hata kama ni katika maeneo yasiyotosheleza huduma kwa abiria na ufinyu wa barabara ambazo kila mwaka bajeti yake haitoshi; zinazaa donda ndugu la msongamano wa magari barabarani katika jiji la Dar es Salaam. Ni lazima tubadili tabia kama taifa.

spot_img

Latest articles

Rais Samia amuasili mtoto mchanga aliyetelekezwa Nzega

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ,Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto...

Beki Yanga afanyiwa upasuaji Afrika Kusini

Na Mwandishi Wetu NAHODHA msaidizi wa timu ya Yanga na mchezaji wa timu ya Taifa...

Rostam aanika maono yake umiliki mpya ya NMG

Na Mwandishi Wetu MFANYABIASHARA na mwekezaji wa Tanzania, Rostam Azizi, ametangaza uwekezaji mkubwa wa kimkakati...

Tanzania Kunufaika na Mradi wa Umoja wa Ulaya wa Kukabiliana na Hatari za Sumu za Kemikali

Na Mwandishi wetu TANZANIA iko katika hatua za awali za upembuzi wa kushiriki katika mradi...

More like this

Rais Samia amuasili mtoto mchanga aliyetelekezwa Nzega

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ,Samia Suluhu Hassan, amemuasili mtoto...

Beki Yanga afanyiwa upasuaji Afrika Kusini

Na Mwandishi Wetu NAHODHA msaidizi wa timu ya Yanga na mchezaji wa timu ya Taifa...

Rostam aanika maono yake umiliki mpya ya NMG

Na Mwandishi Wetu MFANYABIASHARA na mwekezaji wa Tanzania, Rostam Azizi, ametangaza uwekezaji mkubwa wa kimkakati...