Na Winfrida Mtoi
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Steve Barker ameweka wazi kuwa hakuna mechi rahisi ya Ligi Kuu, lakini wamejipanga kuhakikisha wanachukua pointi katika mchezo wao wa kesho dhidi ya KMC utakaopigwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenye jijini Dar es Salaam.
Barker amesema anawaheshimu wapinzani, lakini wamejiandaa na wachezaji wake wanaonekana kujitoa kwa kila mechi na kiwango cha timu kinaendelea kuimarika kila mchezo pamoja na wachezaji wengi wapya.
Amesema baada ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika walirejea kufanya maandalizi mchezo wa kesho ambao ni muhimu kwao kupata ushindi ili kuimarisha nafasi yao katika msimamo wa Ligi Kuu.

“Maandalizi yanakwenda vizuri hadi sasa, tunahitaji kucheza mechi hii vizuri ili kupata ushindi unaotakiwa kama malengo yetu tulijiwekea,” amesema kocha huyo.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa KMC, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema wanajua wanakwenda kucheza mchezo mkubwa, pia bado wana presha kutokana na kuwa katika hali ya chini kwa sababu ya kushindwa kupata matokeo mazuri,
“Kesho tunaingia kwa kutuliza presha kwa mashabiki paamoja na wachezaji wetu, naamini presha itaondoka kutokana na matokeo tutakayopata katika mchezo huo. Kikubwa ni wachezaji kuwa makini,” amesema Bares.
Katika msimamo wa ligi hiyo Simba ipo nafasi ya saba na pointi 16, ikicheza mechi saba, wakati KMC inaburuza mkia na pointi nane ilizokusanya katika michezo 14, ikishinda mechi mbili pekee hadi sasa.


