Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Coastal Union imetembeza kichapo cha mabao 4-1 kwa maafande wa Magereza Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Jumanne, Februari 10, 2025 kwenye dimba la Sokoine, Mbeya.
Mabao ya Coastal Union yalifungwa na Bakari Msimu dakika ya 1, 51, Shiza Kichuya dakika ya 42, na Cleopache Mkandala dakika ya 90+, huku bao la kufutia machozi la Prisons likifungwa na George Mpole dakika ya 45.
Kwa matokeo hali bado ni mbaya kwa Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa. Kwa upande wao, Coastal Union imefikisha pointi 14, ikipanda hadi nafasi ya tisa kutoka nafasi ya 13.

Kocha Msaidizi wa Prisons, Innocent Mwamgonde amesema waliingia uwanjani kwa lengo la kushinda mechi lakini umakini wa wachezaji haukuwa mzuri na wapinzani wao walifanikiwa kutumia makosa waliyofanya na kupata ushindi.
Naye Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya amesema ushindi huo ni zawadi ya uvumilivu wa viongozi na mashabiki wao kwani walipitia kipindi kigumu cha kukosa matokeo mazuri.
Pamba yatakata Mwanza
Katika mchezo mwingine, Pamba Jiji imeibuka na ushindi nyumbani wa bao 1-0 dhidi Namungo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza. Bao hilo likifungwa na Methew Momanyi dakika ya 53.


