Na Winfrida Mtoi
WAKATI Simba kitarajia kukabiliana na Azam FC kesho katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya kombe la Mapinduzi, mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Uganda Steven Mukwala amejiunga kikosi hicho leo na kufanya mazoezi ya mwisho na wenzake.
Mukwala amerejea kikosini baada ya kumaliza majukumu katika timu ya taifa ya Uganda iliyokuwa ikishiriki fainali za kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) ambapo waliishia hatua ya makundi.
Simba imefanya mazoezi ya mwisho katika mazoezi ya mwisho leo Januari 7, 2026 kwenye viwanja vya Maisara, Unguja kujiandaa na mechi hiyo itakayochezwa kesho Alhamisi Januari 8, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, saa 2:15 usiku.

Kuelekea mchezo huo, makocha wa timu hizo mbili zenye upinzani mkali katika Ligi Kuu Tanzania, Steve Barker wa Simba na Florent Ibenge Azam FC wamezungumzia maandalizi yao kuelekea mchezo huo mbele ya waandishi wa habari, huku mmoja akijivunia kikosi chake.
Kocha wa Simba Barker amesema wachezaji wake wana morali ya hali ya juu na wameongezeka kikosini tofauti na walivyoanza, hivyo wamejipanga kucheza vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo ili kutinga fainali ikiwezekana kuchukua taji hilo.
Naye kocha mkuu wa Azam FC, Ibenge ameeleza kuwa anaiheshimu Simba ni kubwa na bora lakini malengo yao katika mechi hiyo ni kuondoka na ushindi.


