Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali imejipanga kuimarisha utendaji wa watumishi wa umma pamoja na kuendeleza mageuzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri Ridhiwani amesema Serikali inalenga kupunguza matumizi ya karatasi na kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya huduma za umma zinatolewa kwa njia ya kidijitali ifikapo mwaka 2050.
Ameeleza kuwa Wizara yake inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi, ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu, mifumo ya utawala bora na uboreshaji wa mazingira ya kazi, sambamba na kutekeleza maelekezo ya Ilani ya CCM na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

“Tathmini ya rasilimali watu imeanza kufanyika katika taasisi za umma ili kubaini mahitaji halisi ya watumishi, hatua hii inalenga kuongeza ufanisi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha ajira zinazingatia weledi na haki,” amesema.
Vilevile, Ridhiwani amesema Ilani ya CCM inaitaka Serikali kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza kipato cha wananchi na kupunguza umaskini, ikiwemo kuzalisha zaidi ya ajira milioni 8.5 kufikia mwaka 2030 katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imetoa vibali 41,500 vya ajira, zikiwamo nafasi 12,000 zilizotolewa kwa mujibu wa ahadi ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, nafasi 5,000 za kada ya afya na 7,000 za ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati,” amesema.

Amebainisha kuwa ajira 12,000 tayari zimetangazwa na waombaji wenye sifa wameitwa kwenye usaili unaotarajiwa kufanyika kesho Disemba 13, 2025 na kwa mara ya kwanza, usaili huo utafanyika katika mikoa yote ili kupunguza gharama kwa waombaji.
Kuhusu Mageuzi ya kidijitali, Ridhiwani amesema Serikali imeanzisha Daftari la Huduma za Serikali (Government Services Directory – GSD), linaloainisha huduma zote za umma, taratibu, gharama, maeneo ya upatikanaji, mawasiliano na namna ya kutoa maoni.
“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu bila wananchi kulazimika kufika ofisini,” amesema, huku akiweka wazi kuwa mageuzi hayo yamelenga kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Aidha amesema Serikali inatarajia kuanza awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN3) chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao utazifikia kaya 507,500 zenye uhitaji mkubwa.
Ameeleza kuwa awamu hiyo itaanza mapema mwaka 2026 baada ya kukamilika kwa awamu ya pili Septemba mwaka huu.“PSSN3 inatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 296, zitakazotolewa na Benki ya Dunia, Serikali ya Tanzania na wadau wengine wa maendeleo,” amesema.


