Na Mwandishi Wetu
Mabishano ya ushabiki wa Yanga na Simba yamesababisha kifo cha mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Evaristo Mwambogolo (28), mkulima na mkazi wa Ululu wilayani Mbozi mkoani Songwe, baada ya kuchomwa kisu kifuani na mtu aliyejulikana kama Exavery Mwaweza.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi mkoani humo, imesema Mwambogolo alifariki dunia akiwa njiani wakati akikimbizwa Zahanati ya Iyula kwa ajili ya matibabu.
“Uchunguzi wa awali umeonesha chanzo cha tukio hilo ni ushabiki wa mpira wa timu ya Simba na Yanga kati ya marehemu na mtuhumiwa, ambapo mtuhumiwa alitumia kisu alichokuwa nacho wakati wa ugomvi huo, mara baada ya kutenda kosa hilo, alitoroka kusikojulikana, ” imesema taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi hilo limesema linafanya msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa huyo ili akamatwe na aweze kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.