Na Mwandishi Wetu
Timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu Tanzania ‘Tembo Warriors’ imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAAF) baada ya leo kuichapa Uganda mabao 4-1 katika michuano hiyo inayoendelea nchini Burundi.
Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Tembo Warriors Ivo Mapunda, amesema ushindi huo umetokana na marekebisho ya kiufundi waliyofanya baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kenya.
Amesema ilikuwa ni mechi ngumu lakini walipambana kwa sababu ilikuwa ni lazima washinde ili kuendelea na hatua nyingine ya mashindano.

” Leo ilikuwa ni lazima tushinde, nawashukuru wachezaji kwa kufuata maelekezo vizuri, tunachoangalia kwa sasa ni mchezo wetu wa kesho na Burundi ambao ni lazima tushinde ili tuingie fainali,” amesema Mapunda.
Mchezo wa kwanza timu hiyo ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 na Kenya ambayo ndiyo inayoongoza kundi B ikiwa na pointi sita, Tanzania ya pili na alama tatu.