Na Mwandishi Wetu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetuma barua ya malalamiko kwa Shirikisho la Soka la Kimataifa(FIFA), ikilitaka kuifanyia uchunguzi klabu ya Yanga kuhusu kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Malalamiko ya Chadema yametokana na Yanga kushiriki katika harambee ya kuchangia fedha za kufanikisha kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025 iliyofanyika Agosti 12, 2025, ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ambapo klabu hiyo ilichangia sh 100 milioni.
Kupitia barua hiyo, Chadema pia imeomba kuchukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na Kanuni kwa maofisa na viongozi wa klabu hiyo waliohusika katika jambo hilo la uchangiaji kwa madai kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni na sheria za FIFA.
“Sisi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa heshima tunawasilisha malalamiko rasmi na ombi kuhusu mwenendo wa Young African Sports Club (“Yanga”) ya Tanzania, ambapo vitendo vya hivi karibuni ni ukiukaji wa moja kwa moja wa misingi ya FIFA,”
Mkurugenzi wa Mkurugenzi wa Masuala ya Nje na Diaspora wa Chadema, John Kitoka amethibitisha kuandika barua hiyo na kusema tayari imepokelewa FIFA.
Hivi karibuni baada ya kuibuka mjadala juu ya Yanga kuchangia CCM kwa sababu mashaki wake wana itikadi za vyama tofauti tofauti, uongozi wa klabu hiyo ulitoa taarifa ya ufafanuzi kuwa fedha zilizotolewa katika uchangiaji huo zimetoka Taasisi ya GSM Foundation na sio za mfuko wa wanachama.


