Na Tatu Mohamed, Dodoma
MFUGAJI na mtaalamu wa kilimo na mifugo kutoka jijini Dodoma, Christopher Dioniz, ametambulisha aina ya kuku wa kipekee wa kisasa wanaojulikana kama Ayam Cemani kutoka Indonesia, ambao sasa wanapatikana jijini Dodoma.
Akizungumza l katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Dioniz amesema kuwa kuku hao si wa kawaida, bali wanajulikana kwa thamani yao kubwa ya kiafya na lishe, hasa katika mataifa ya Indonesia na China.
“Kuku wa Ayam Cemani wanaaminika kusaidia afya ya binadamu kutokana na virutubisho vya pekee vilivyopo kwenye nyama yao,” amesema.

Aidha, Dioniz amesema kuwa anajihusisha pia na ufugaji wa kuku wa kienyeji, huku akibainisha kuwa moja ya mafanikio yake yanatokana na matumizi ya chakula cha kuku chenye ubora wa hali ya juu kinachoitwa Rehoboth Animal Feeds, kinachozalishwa na timu yake jijini Dodoma.
“Tunatengeneza chakula kulingana na mahitaji ya aina mbalimbali za kuku wa kienyeji, wa nyama, na chotara. Pia tunatoa mafunzo ya kutengeneza chakula hicho kwa kutumia fomula maalum pamoja na elimu ya ufugaji wa kuku kwa ujumla,” ameongeza.
Mbali na hilo, Dioniz amesema kuwa wanauza pia vifaa vyote vinavyohitajika katika ufugaji wa kuku, na katika maonesho hayo wamewasilisha bidhaa mbalimbali za vyakula vya mifugo kwa ajili ya kuwahudumia wafugaji wanaotafuta ubora.

Ametoa wito kwa wafugaji kote nchini kuhamia katika mfumo wa ufugaji wa kisasa unaozingatia lishe bora na mbinu sahihi za utunzaji wa kuku, ili kuongeza tija, afya ya mifugo na kipato chao kupitia sekta ya mifugo.