Na Mwandishi Wetu
Mfanyabiashara na mwekezaji Rostam Azizi, amesema kuna haja ya serikali na wafanyabiashara wenzake kufikiria kujikita zaidi katika sekta ya habari za kidigitali ‘Digital Media’ na matumizi ya akili mnemba (AI), ikiwamo kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania ili kuendana na mazingira ya sasa.
Rostam ameyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa jana Julai 15,2025 na mwandishi wa habari mwandamizi nchini ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Media Brains, Absalom Kibanda kwenye Mkutano wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika unaofanyika jijini Arusha ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango.


Ameeleza kuwa katika zama hizi mpya tasnia ya habari imetawaliwa zaidi na mitandao ya kijamii matumizi ya AI, sehemu ambayo ni kimbilio na tegemeo la kwanza la jamii kupata na kusambaza habari.
Hata hivyo amesema changamoto iliyopo katika mazingira ya upashaji wa habari ya sasa, ni uwepo wa maudhui mengi yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi bali yanazalishwa na kusambazwa na watu walioko nje ya mipaka ambao hawawezi kuguswa na sheria, mila, misingi ya jamii ya Tanzania.

Amesema kuwa watu hao mara nyingi hawana hisa katika amani ya nchi, hawana uwekezaji katika maendeleo na hawawajibiki kwa madhara ya maneno yao.
Kutokana na hali hiyo, Rostam amesema Tanzania inapaswa kuwezeshwa kumiliki na kuendesha majukwaa ya kisasa, yanayoweza kushindana katika uwanja wa kidijitali kwa kutumia ukweli, utu, ubunifu, na muktadha halisi wa Kitanzania.
“Tunahitaji kuwajengea uwezo vijana wetu wa habari za kidijitali, wabunifu wa mitandao, wataalamu wa data na artificial intelligence (AI) — ili waweze kutoa habari na kusimulia simulizi ya taifa letu kwa macho yetu, kwa sauti yetu, na kwa misingi yetu.
“Ninazungumzia haya si tu kama mfanyabiashara, wala si tu kama raia, bali kama mtu anayeamini kuwa roho ya taifa inaweza kujengwa au kubomolewa na uadilifu wa mazingira ya habari katika jamii yetu.
“Tunaishi katika zama mpya ambapo vita si tena kwenye uwanja wa mapambano wa kawaida, bali vinafanyika mtandaoni. Silaha siyo tena ni bunduki, bali algorithms. Kila simu ya mkononi imekuwa kipaza sauti. Kila “like” au “share” kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ni kura ya maoni. Na kila uongo usiopingwa, hatimaye huwa sehemu ya majadiliano ya taifa na hatimaye kuwa sehemu ya kumbukumbu ya taifa.
“Katika mazingira haya mapya, vyombo vya habari si tu vinakuwa mhimili wa nne kama tulivyozoea kusema bali vimekuwa ndiyo kimbilio na tegemeo la kwanza la jamii kupata na kusambaza habari, hasa wakati wa mivutano ya kisiasa, majaribu ya kijamii, au mitafaruku ya kitaifa.
Amesema watu wanawekeza katika mahoteli na miundombinu, lakini katika imesahalulika miundombinu ya habari na simulizi ambapo fikra, mitazamo na hulka za kizazi kipya zinafinyangwa kila siku.
“Tunajenga viwanda, lakini tunasahau kuwa viwanda vya mtandaoni ndivyo vinavyozalisha mitazamo ya kisiasa, maadili ya kijamii, na taswira ya taifa letu ndani na nje ya mipaka yetu.
Amefafanua kuwa halo yakifanyika, yataifanya Tanzania kuwa kinara si tu katika ukuaji wa uchumi, bali pia katika ubunifu wa vyombo vya habari, matumizi ya AI kwa maudhui ya maadili, na usimuliaji wa simulizi za kizalendo kwa njia shirikishi na za kidemokrasia.