Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Kawe anayemaliza muda wake na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amesema hawezi kukaa kimya endapo vitendo vya utekaji vitaendelea nchini, huku akisisitiza kuwa bado ni mwanachama thabiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 16, 2025, Askofu Gwajima amesema licha ya baadhi ya watu kumtuhumu kwamba ana nia ya kuhamia vyama vya upinzani, yeye bado yupo CCM kwa dhati na hatarajii kutoka, bali atasimama ndani ya chama hicho kutetea ukweli.
“Siwezi kuacha kuzungumza kama watu wataendelea kutekwa. Nipo CCM na nitaendelea kuwepo. Hakuna kutoka wala kugombana, tutabanana humu humu na tutaendelea kushauriana,” amesema Askofu Gwajima.

Hata hivyo, Askofu Gwajima amesisitiza kuwa hajawahi kusema kama CCM ndiyo inateka watu, lakini kama chama kilicho madarakani, kina wajibu wa kuhakikisha haki, amani na maridhiano vinapatikana nchini.
Akizungumzia msimamo wa Chadema kuhusu kutoshiriki Uchaguzi Mkuu bila kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi (reforms), Askofu Gwajima amesema ni busara kwa CCM kama chama tawala kuhakikisha maridhiano yanapatikana ili Taifa lisigawanyike.
“Tunaweza kushinda uchaguzi bila Chadema, lakini je, tutawezaje kuitawala nchi iliyogawanyika kwa misingi ya uchaguzi usioaminika? Ni bora tukakubaliana kwenye baadhi ya reforms, tukaingia wote, kisha tuwashinde kwenye uwanja wa haki,” amesema.

Askofu Gwajima amesema si busara kuendekeza ushindi wa kisiasa kwa gharama ya mshikamano wa kitaifa, na kuhimiza CCM kutanguliza maslahi ya Taifa kabla ya maslahi ya kisiasa.
“Tuwe na nchi iliyoungana baada ya uchaguzi. Hapo ndipo Rais anaweza kuongoza kwa amani na kuleta maendeleo. Nchi huja kwanza, vyama vinakuja baadaye,” ameongeza.
Ameishauri CCM na Serikali kutafuta njia ya busara ya kuafikiana na Chadema kuhusu madai ya reform, kwa lengo la kupata ushindani wa haki na taifa lenye mshikamano baada ya uchaguzi.