Baba Levo atembelea Banda la TTCL Sabasaba, apongeza Mapinduzi ya Kidijitali

Na Mwandishi Wetu

MSANII na mtangazaji maarufu nchini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, ambaye pia ni Balozi wa Kampeni ya Walete ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ametembelea banda la shirika hilo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Baba Levo alipata fursa ya kuzungumza na wateja, kuhamasisha matumizi ya huduma za TTCL, sambamba na kuelezea mchango mkubwa wa shirika hilo katika mageuzi ya kidijitali nchini.

Pia alitumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi zake za kulijengea uwezo shirika hilo ili liendelee kuwa mhimili imara wa mawasiliano kwa Watanzania.

Ujio wa Baba Levo uligubikwa na hamasa kubwa kutoka kwa wananchi na mashabiki waliokusanyika kwa wingi kushuhudia msanii huyo akiungana na watumishi wa TTCL kutoa elimu kuhusu huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo lenye historia ndefu nchini.

Akizungumza na wataalamu wa TTCL waliopo kwenye banda hilo, Baba Levo alionesha kufurahishwa na hatua mbalimbali za kiteknolojia zinazotekelezwa na shirika hilo.

Alitaja mafanikio kama usambazaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, uanzishaji wa Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (Data Center), upatikanaji wa intaneti ya kasi, huduma za simu pamoja na vifaa vya kisasa kama modemu, MiFi na huduma ya faiba mlangoni inayowezesha matumizi ya vifaa vya nyumbani kwa njia ya kidijitali.

“TTCL ni alama ya taifa. Tunapaswa kujivunia kuwa na taasisi ya kizalendo inayohakikisha Watanzania wanapata mawasiliano salama, ya uhakika na kwa gharama nafuu,” amesema Baba Levo.

Kwa upande wake, Meneja wa Banda la TTCL ambaye pia ni Meneja Bidhaa, Bi. Janeth Maeda, alisema ziara ya Baba Levo ni uthibitisho wa mshikamano baina ya taasisi za umma na wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

“Tunamshukuru Baba Levo kwa kutenga muda wake kutembelea banda letu. Ni ishara kuwa jamii inatambua umuhimu wa TTCL kama taasisi ya umma inayotekeleza dhamira ya Serikali ya kuwafikishia Watanzania huduma bora za mawasiliano,” amesema Maeda.

Maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Maonesho ya Biashara ya Kimataifa – Sabasaba, Fahari ya Tanzania”.

TTCL imeendelea kuonesha namna huduma zake zinavyounga mkono ajenda ya taifa ya kidijitali, huku ikiwahakikishia wateja wake huduma zenye usalama, ubora na unafuu wa gharama.

spot_img

Latest articles

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

Padre aliyepotea apatikana akiwa hai

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumpata Padre Camillus Nikata wa Jimbo...

Waangalizi wa Uchaguzi watakiwa kutoingilia mchakato wa Uchaguzi Mkuu

Na Mwandishi wetu, Dodoma WAANGALIZI wa Uchaguzi wa ndani na wa kimataifa wametakiwa kuzingatia sheria...

More like this

Mwanamke ashikiliwa  Polisi kwa  kumuua mume wake na kumfukia ndani ya nyumba yao

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina...

Padre aliyepotea apatikana akiwa hai

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kumpata Padre Camillus Nikata wa Jimbo...