Malalamiko 461 Yawasilishwa EWURA Kwa Miaka Miwili

Na Tatu Mohamed 

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema katika kipindi cha miaka miwili, yaani 2023/24 na 2024/25, imesajili jumla ya malalamiko 461.

Imefafanua kuwa, kati ya hayo, malalamiko 167 (asilimia 36) yalihusiana na huduma zinazotolewa na Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira huku malalamiko 45 (asilimia 27) yalitoka kwa wateja wa DAWASA, na kati ya hayo, 27 (asilimia 60) yalihusu masuala ya bili za maji.

Hayo yamebainishwa leo Juni 25, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Mwainyekule wakati akifungua semina kwa Maofisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA.

Amesema lengo la semina hiyo ni kupunguza idadi kubwa ya malalamiko yanayofikishwa EWURA, hasa yale yanayohusu masuala ya bili za maji.

“Takwimu hizi zinaonyesha wazi kwamba endapo DAWASA itatatua kikamilifu malalamiko ya wateja wake, idadi ya malalamiko yanayofikishwa EWURA itapungua kwa kiasi kikubwa. 

“Hii ndiyo sababu kuu iliyoisukuma EWURA kuandaa semina hii kwa maafisa huduma kwa wateja wa DAWASA, ikilenga kuwakumbusha wajibu wao katika kushughulikia malalamiko ya wateja. Ikumbukwe kuwa uamuzi wa baadhi ya malalamiko yanayoletwa EWURA huambatana na gharama kwa DAWASA,” amesema.

Amefafanua kuwa, kupunguza au kuondoa malalamiko yanayowasilishwa na EWURA ni kwa maslahi ya DAWASA na watoa huduma wote wanaodhibitiwa na EWURA.

Amesema kwa miaka mingi, Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maji na usafi wa mazingira ambapo hadi kufikia Disemba 2024, idadi ya watu waliofikiwa na mtandao wa maji safi ilifikia asilimia 91.6 kwa mijini na asilimia 83 kwa vijijini, kulingana na hotuba ya Waziri wa Maji wakati wa kuwasilisha bajeti ya wizara kwa mwaka 2025/26.

Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha Mamlaka za Maji zinaboresha huduma zake, EWURA iliunda Kanuni za Masuala ya Leseni na Ubora wa Huduma za Mwaka 2020 ambapo miongoni mwa matakwa ya Kanuni hizo ni kuhakikisha kuwa kila Mamlaka ya Maji inakuwa na Mkataba wa Huduma kwa Wateja. 

“Hata hivyo, kuna changamoto kwamba baadhi ya Mamlaka za Maji zinawaficha wateja wao kuhusu uwepo wa Mikataba hiyo. Kutokana na hali hiyo, naagiza Mamlaka zote za Maji kuhakikisha Mikataba yao ya Huduma kwa Wateja inawekwa wazi kwenye tovuti zao na inapatikana katika ofisi zao zinazotoa huduma kwa wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja DAWASA, Ritamary Lwabulinda amekiri kuwa wanapokea malalamiko mengi na wanaendelea kuyafanyia kazi.

“Tunawashukuru EWURA kwa semina hii ambayo ni ya kukumbushana tu, kwani mambo yote tunayojifunza tayari yapo kwenye Mkataba wetu wa huduma kwa wateja.

“EWURA, kama mdhibiti, inaweza kusikia malalamiko mengine kutoka kwa wateja ambayo DAWASA pengine haijayasikia hibyo Mazungumzo na EWURA yatasaidia DAWASA kufanya vizuri zaidi katika kutoa huduma,” ameongeza.

spot_img

Latest articles

TCAA YAIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA KUPITIA DAWATI MAALUM

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kupitia kwa Mkurugenzi wake...

VETA yajivunia ushindi, yaeleza mchango wa Mafunzo ya Ufundi Stadi

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema ushindi...

Twange: Tanesco yazidi kupanua Nishati Safi ya kupikia, kuimarisha usambazaji wa umeme Zanzibar

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema Shirika...

WANANCHI WAENDELEA KUNUFAIKA NA OFA ZA TTCL SABASABA 2026

Na Mwandishi Wetu MAAFISA wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wanaendelea kuwahudumia wananchi wanaotembelea...

More like this

TCAA YAIMARISHA HUDUMA KWA WATEJA KUPITIA DAWATI MAALUM

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kupitia kwa Mkurugenzi wake...

VETA yajivunia ushindi, yaeleza mchango wa Mafunzo ya Ufundi Stadi

Na Mwandishi Wetu MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema ushindi...

Twange: Tanesco yazidi kupanua Nishati Safi ya kupikia, kuimarisha usambazaji wa umeme Zanzibar

Na Mwandishi Wetu MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema Shirika...