Na Mwandishi Wetu
MAMIA ya wananchi, viongozi wa Serikali na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama leo (Jana) walikusanyika katika Viwanja vya Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma kushiriki Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mashujaa, yaliyongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yalitawaliwa na shughuli za kuenzi mchango wa mashujaa waliopigania uhuru wa Tanzania na wale waliojitolea kulinda amani, umoja na mipaka ya nchi, ambapo Rais Samia aliwaongoza viongozi mbalimbali kuweka mashada ya maua katika Mnara wa Mashujaa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi za juu akiwemo Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Tanzania, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, viongozi wastaafu wa Serikali, mawaziri, mabalozi na viongozi wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Mbali na uwekaji wa mashada ya maua, viongozi hao walishiriki pia kuweka alama za jadi zikiwemo shoka, mkuki na upinde kama ishara ya ushujaa, uzalendo na dhamira ya kuendelea kuilinda Tanzania.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Idara ya Uhamiaji vilifanya gwaride maalumu la heshima lililoambatana na salamu za kijeshi, huku wananchi waliojitokeza kwa wingi wakishuhudia tukio hilo la kitaifa.

Maadhimisho hayo yalipambwa pia na burudani kutoka kwa vikundi vya sanaa na Bendi ya JWTZ, ambazo ziliwasilisha nyimbo zenye ujumbe wa uzalendo, umoja na kuenzi historia ya ukombozi wa Taifa.

Siku ya Mashujaa huadhimishwa kila mwaka Julai 25 ikiwa ni siku ya kutambua na kuthamini mchango wa Watanzania waliojitolea kwa ajili ya uhuru, ulinzi wa nchi na maendeleo ya Taifa.

Maadhimisho ya mwaka huu yameendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na kuendeleza tunu za uzalendo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.



