Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewaeleza wabunge na madiwani hususan waliokuwa wanajifungia vioo kwenye magari wajue wakati umefika.
Amesema uchaguzi mkuu sio ajali na kwamba wabunge na madiwani wanajua kila baada ya miaka mitano hufanyika uchaguzi mkuu.
Aidha, amewaeleza wana CCM wanaotaka kugombea ubunge na udiwani ni vema wakapima uwezo wao kama ambavyo unapaswa kupima kina cha maji kwa fimbo kabla ya kuvuka mto kusombwa na maji.

Akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, leo Juni 23, 2025, Wasira ametumia nafasi hiyo kuwataka wana CCM kujiandaa kwenda kutiki ifikapo Oktoba na kwa nafasi ya urais tayari Chama kimepitisha jina la Dk. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza ni Dk. Emanuel Nchimbi.
“Kwa upande wa urais tumemaliza tumeshaweka mgombea wetu Dk.Samia Suluhu Hassan na kazi yetu ni kumuuza kwa wananchama na wananchi .Kwa wabunge kama ubunge unaisha Juni 27 ndio maana hauwapi presha maana tangu walipoingia maana walijua ikifika miaka mitano uchaguzi unafanyika.
“Kwa hiyo uchaguzi sio ajali kama wewe unauogopa labda hukufanya maandalizi maana wako watu katika jamii hata wale waliowachagua hawawajui wale ndio wenye kupata presha… sasa kama unafunga vioo unawapita watu usilaumu watu,” amesema.
Ameeleza kuwa amekuwa bungeni kwa miaka 30, hivyo analijua bunge vizuri na kueleza kwamba ubunge unavyopatikana unapatikana kwa kujenga uhusiano na watu, ukijenga uhusiano na watu mambo yako yanakuwa rahisi
“Kazi yangu si kumpigia mtu debe mbunge ila ukifika kwa wana wana CCM na lakini ukifika hapa kwa mfano unasikia kaulimbiu za wananchi au wana CCM wanamtaja wanayemtaka.Kwa wabunge ambao walifanya kazi zao vizuri wala hawana wasiwasi,” ameeleza Wasira.
Pia Wasira amesema uchaguzi umefika na wanachama wana haki ya kuchukua fomu ila alishauri kwa wale wanachama wapya wanaotaka ubunge wakapima nguvu ya waliopo au waliomaliza muda wao.