Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejidhatiti kujenga uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na za uhakika za mawasiliano.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kikihusisha wahariri na waandishi wa habari.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi Mwasalyanda amesema dhamira ya Serikali ni kuwawezesha Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kupitia fursa za teknolojia na mawasiliano ya kisasa.
“Mawasiliano ni sawa na maji, ni sawa na umeme. Katika uchumi wa kidijitali tunahitaji kila mwananchi awe na huduma ya mawasiliano ya uhakika. Mfano, mkulima wa Sumbawanga aweze kupata taarifa za soko kutoka Kariakoo kwa haraka,” amesema.
Mhandisi Mwasalyanda amesema kuwa UCSAF kwa sasa inatekeleza miradi 15 ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa lengo la kuimarisha huduma hiyo katika maeneo yote nchini, hasa ya vijijini.

Ameeleza kuwa ujenzi wa minara 758 unaendelea, mradi ambao Serikali imetoa ruzuku ya jumla ya Shilingi bilioni 126 ili kuhakikisha wananchi waliokuwa hawajafikiwa na huduma hizo sasa wanapata mawasiliano ya uhakika.
Katika hatua nyingine, UCSAF imeanza kutekeleza mradi wa usambazaji wa huduma za intaneti ya bure katika maeneo ya wazi, ambapo mpaka sasa huduma hiyo imefungwa katika vituo saba na maeneo 17 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba).
Mafunzo ya TEHAMA kwa walimu na vifaa kwa shule maalumUCSAF pia imejikita katika kuwawezesha walimu nchini kupata mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambapo mpaka sasa walimu 3,798 kutoka shule 1,791 wamepatiwa mafunzo hayo.

Kati yao, walimu 326 wanatoka Zanzibar na 3,180 kutoka Tanzania Bara. Mafunzo hayo yanatolewa kwa kushirikiana na vyuo vya MUST, DIT na UDOM.Vilevile, Mfuko huo umepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 22 za wanafunzi wenye mahitaji maalum, mradi ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.8.
Kwa mujibu wa UCSAF, juhudi hizi zinaendana na dira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika mapinduzi ya teknolojia.


