Tundu Lissu Arejeshwa Gerezani hadi Juni 2, mwaka huu

Na Mwandishi Wetu

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amerejeshwa rumande hadi Juni 2, 2025, baada ya kesi yake ya uhaini na ile ya kuchapisha taarifa za uongo kuahirishwa kwa mara nyingine, Mahakama ikielezwa kuwa upelelezi uko katika hatua za mwisho.

Lissu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo, Jumatatu Mei 19, 2025, ambapo wanachama na viongozi wa Chadema walijitokeza kwa wingi kushuhudia mwenyekiti wao akiendelea kusikilizwa mahakamani.

Kesi hiyo ya uhaini iko mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franko Kiswaga, ambapo upande wa mashtaka, ukiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, uliiambia mahakama kuwa bado upelelezi haujakamilika lakini uko katika hatua za mwisho.

“Kwa sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha upelelezi, tunaiomba mahakama itupe muda wa siku 14 zaidi,” amedai Katuga.

Katika hatua nyingine, Mahakama hiyo imetoa uamuzi mdogo wa kwamba kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kwa njia ya kawaida na si kwa njia ya mtandao kama ilivyokuwa ikipendekezwa awali.

Aidha, Mahakama imeagiza kuwa tarehe ijayo itafanyika tathmini ya usalama wa eneo la mahakama ili kubaini kama kuna tishio lolote linalohatarisha usalama wa mshtakiwa.

“Kama hakutakuwa na tishio lolote la kiusalama, basi mshtakiwa ataendelea kusimama kizimbani mwenyewe bila kuwa chini ya ulinzi wa karibu wa askari magereza,” amedai Hakimu Kiswaga.

Pia, Mahakama imewakumbusha washiriki wote wa kesi hiyo, wakiwemo wafuasi wa Chadema kuhakikisha kuwa hakuna kelele wala mihemko mahakamani, akisisitiza kuwa heshima ya mahakama lazima ilindwe wakati wote.

Serikali Kuleta Mashahidi 15

Mbali na kesi ya uhaini, Lissu anakabiliwa na kesi nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo, ambapo Mahakama imesikia maelezo ya awali (PH) mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini.

Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali Katuga ameieleza Mahakama kuwa upande wa mashtaka unatarajia kuwasilisha mashahidi 15 na vielelezo tisa ili kuthibitisha mashtaka dhidi ya Lissu.

Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Peter Kibatala na Rugemeleza Nshala wamedai hawako tayari kutaja idadi ya mashahidi wao kwa sasa.

Wakati akisomewa maelezo ya awali, Lissu alikubali baadhi ya taarifa binafsi ikiwemo jina, makazi yake ya Tegeta, na kwamba ni Mwenyekiti wa Chadema, lakini alikana mashitaka yote matatu ya kuchapisha taarifa za uongo.

Alikana madai kuwa alitoa taarifa kwamba wagombea wa Chadema walienguliwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 kwa maelekezo ya Rais, na pia alikana kutoa kauli kwamba majaji wa Mahakama ni wafuasi wa CCM wasioweza kutoa haki, akidaiwa kuchapisha kauli hizo kupitia mtandao wa YouTube.

Mwisho

spot_img

Latest articles

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

PURA yajivunia mafanikio katika Ajenda ya Nishati Safi na ushiriki wa Watanzania Sekta ya Mafuta na Gesi

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia...

Machungu, damu yamwagwa tena

Maadhimisho ya Saba Saba nchini Kenya ni tukio muhimu katika kukumbuka mapambano ya kudai...

eGA yatumia Sabasaba kuelimisha umma kuhusu Mfumo wa e-Mrejesho, yajivunia Tuzo ya Kimataifa

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Serikali Mtandao (eGA) imeendelea kuonesha namna ambavyo Serikali inavyotekeleza mageuzi...

More like this

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

PURA yajivunia mafanikio katika Ajenda ya Nishati Safi na ushiriki wa Watanzania Sekta ya Mafuta na Gesi

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia...

Machungu, damu yamwagwa tena

Maadhimisho ya Saba Saba nchini Kenya ni tukio muhimu katika kukumbuka mapambano ya kudai...