Na Tatu Mohamed, Media Brain
KATIKA juhudi za kukuza uzalishaji wa ndani wa mbolea na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni ya ESSA ya Indonesia, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea ya Urea.

Makubaliano hayo yatasaidia kuhakikisha upatikanaji wa gesi asilia kama malighafi muhimu ya kutengeneza mbolea, huku TPDC ikishiriki siyo tu kama msambazaji wa gesi, bali pia kama mwekezaji katika mradi huo.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini, Derrick Moshi ambaye ni Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC, amesema hatua hiyo ni mwanzo wa safari muhimu ya kuimarisha uzalishaji wa ndani wa mbolea nchini.
“Tumesaini makubaliano ya ESSA kutekeleza azma ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea nchini. Sisi kama TPDC hatutaishia kuwa wasambazaji wa gesi tu, bali tutashiriki kama wawekezaji wa moja kwa moja kwenye safari hii,” amesema Moshi.
Ameeleza kuwa ESSA imepata kibali kuanza tafiti za kina kuhusu mahitaji ya gesi, gharama na miundombinu ya kuipeleka kiwandani.
“Tunawahakikishia kwamba kwa visima tulivyonavyo sasa, suala la gesi kwa ajili ya kuzalisha mbolea ni jambo linalowezekana. TPDC imejipanga katika mipango ya muda mfupi na mrefu kuweka akiba ya gesi kwa ajili ya viwanda vya mbolea, jambo linaloonyesha dhamira ya kweli ya kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani ya kilimo nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Kamishna na Mjumbe wa Bodi ya ESSA, Rahul Puri, amesema mradi huo wa miaka mitano unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 1.3, sawa na Shilingi trilioni 3.5 za Kitanzania.
Amesema ujenzi wa Kiwanda hicho Mkoani Mtwara, utafanyika kwa awamu tatu hadi kukamilika kwake, huku kikitarajiwa kuzalisha tani milioni moja za mbolea kwa mwaka.
“Mahitaji ya gesi ni takribani futi milioni 70 kwa siku. N tukuishakamilisha asilimia 60 ya mbolea itabaki nchini, na asilimia 40 itauzwa nje ya nchi,” amesema Puri.
Aidha, amesema mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 5,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 300,000, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa kiuchumi wa Watanzania.
Dkt. Anthony Diallo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ni hatua ya msingi katika kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi.
“Kwa sasa, mbolea nyingi hasa Urea tunaiagiza kutoka nje. Tukianza kuzalisha hapa nchini, tutakuwa na uhakika wa kujitegemea kwenye pembejeo muhimu za kilimo,” amesema.
Amefafanua kuwa, mwaka uliopita Tanzania iliagiza takribani tani 800,000 za mbolea, lakini mahitaji yameongezeka hadi kufikia zaidi ya tani milioni moja, ambayo bado hayatoshelezi wakulima waliopo nchini.
Awali, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Lameck Borega amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa uchumi wa taifa.
“Mwaka uliopita tulitumia zaidi ya dola milioni 50 (sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 120) kuagiza mbolea kutoka nje. Fedha hizi zingetumika ndani ya nchi kwenye miradi ya maendeleo,” anasema Borega.
Ameongeza kuwa ujio wa kiwanda cha ndani utarahisisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati, kupunguza gharama za usafiri, na hivyo kuondoa hitaji la serikali kutoa ruzuku kwa wakulima.
“Tukiwa na kiwanda chetu, bei itashuka, na mkulima atapata mbolea kwa gharama nafuu na kwa wakati,” anasema Borega.
Mradi huu wa kiwanda cha mbolea unaoongozwa na TPDC na ESSA ni moja ya miradi ya kimkakati inayodhihirisha dhamira ya Tanzania kuwekeza katika sekta ya kilimo. Kupitia mradi huu, nchi itanufaika na ajira, kuongezeka kwa tija ya kilimo, kupungua kwa uagizaji wa nje, na kuimarika kwa uchumi wa ndani.