Na Mwandishi Wetu
Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema hauko yatari kupeleka shauri kwenye Kamati za Mamlaka za soka ndani kama iliyoelekezwa na Mahakama ya Kimataifa ua Usuluhisi wa Michezo (CAS), ikihofia dhuluma, huku ikisisitiza kutocheza mechi ya’derby’.
CAS ilielekeza Yanga kurudi kwenye Kamati za ndani kabla ya kurudi katika mahakama hiyo kwa ajili ya rufani.
Katika taarifa ambayo klabu hiyo imeitoa leo Mei 5, 2025imesema msimamo wao juu ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Bara uko pale pale wa kutoshiriki mechi hiyo kwa namna yoyote.

“Kutokana na uonevu na uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo wa dhahiri kwa baadhi ya timu unaondelea kufanywa na Mamlaka za soka Tanzania, Uongozi wa Yanga hauna imani na hauko tayari kupeleka shauri hilo kwenye Mamlaka ambao zinatenda dhulma,” imesema.
Kupitia Taarifa hiyo,uongozi wa Wanajangwani hao,umewataka Wanayanga kuwa tayari kuipambania haki yao kivyovyote vile ili kukomesha dhuluma na uvunjwaji wa kanuni unaondelea kwa maslahi mapanda ya soka nchini.
Ikumbukwe kuwa Yanga ilifungua shauri la madai CAS kwa kutoridhishwa na kitendo cha kuahirishwa kwa mchezo wake dhidi ya Simba uliokuwa uchezwe Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga iliwasilisha shauri la kuomba mechi hiyo isipangiwe tarehe nyingine hadi uamuzi utakapotolewa na Makahama hiyo. Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na Klabu ya Simba.
Hata hivyo CAS iliijibu Yanga kwa kuitaka kurudi katika Kamati za Mamlaka za soka ambapo muda mfupi baadaye Bodi ya Ligi ilitangaza kutoa ratiba mpya ya Ligi Kuu ikiwamo mchezo huo uliahirishwa wa Yanga na Simba.