Na Mwandishi Wetu
BODI ya Kampuni ya Misitu (MCL), kampuni tanzu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeanza rasmi kazi zake na kupewa matarajio tisa ya utekelezaji kutoka kwa Bodi ya Ushauri ya TFS.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha utambulisho wa bodi hiyo, kilichofanyika leo mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Meja Jenerali Dkt. Mbaraka Mkeremy, amesema Kampuni ya Misitu ilianzishwa kama mkakati wa kibiashara wa TFS kwa lengo la kuanzisha na kuendeleza miradi ya kibiashara inayotumia rasilimali za misitu na nyuki.
“Lengo kuu la miradi hii ni kuongeza mapato ya Wakala na kupanua biashara zinazotegemea rasilimali za misitu na nyuki,” alisema Meja Jenerali Mkeremy.

Ameongeza kuwa kampuni hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa mapendekezo ya miradi, kushughulikia mipango ya uwekezaji, na kupunguza utegemezi wa Wakala kwa Serikali.
“Hivyo kipimo chetu kitakuwa ni kiwango cha mapato kinachoongezeka kwa taasisi kutokana na kazi za kampuni,” amesisitiza Mkeremy.
Matarajio tisa yaliyotajwa na Bodi ya Ushauri ya TFS kwa Kampuni ya Misitu ni pamoja na kuimarisha utendaji wa kibiashara, kuongeza thamani ya mazao ya misitu, kuongeza mapato, na kuboresha huduma na bidhaa.

Mengine ni kukuza ubunifu na matumizi ya teknolojia, kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali, kusimamia sheria na taratibu, kukuza ujuzi na mafunzo kwa watumishi, pamoja na kuhimiza weledi na uaminifu katika utendaji wa kazi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Misitu, Fortunatus Mhambe, alishukuru kwa maelekezo yaliyotolewa na Bodi ya Ushauri ya TFS, na kwa niaba ya wajumbe wenzake aliahidi kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo na bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Wajumbe wengine wa bodi hiyo ni Neema Mbise, Peter Mwakosya, Prof. Yonika Nganga, na Chelestino Balama. Katibu wa Bodi ni Bi. Salome Rwiza.

