JUMATATU wiki hii nilipata wasaa wa kuingia katika mazingira kilipokuwa kiwanda cha nguo cha Urafiki kikijulikana kama Urafiki Textile. Hiki ni kiwanda kikubwa kilichovuma sana miaka ya 70 na 80 kwa kiasi fulani, kikizalisha nguo, hasa kanga. Vazi linalopendwa sana na wanawake. Nikiwa ndani ya mazingira ya kilichokuwa kiwanda hicho, nijisikia mnyonge sana.
Unyonge huu si wa kitu kingine bali ni kuona jinsi ambavyo fursa kubwa ya kutengeneza ajira, kujenga uchumi kwa ajili ya watu wetu imetupwa. Yaani mle ndani kama ambavyo wengi wanaelewa, ni mahame. Hakuna kitu chochote kinachoendelea mbali ya baadhi ya majengo kukodishwa kama maghala ya bidhaa kutoka nje.
Nikakumbuka mwaka jana Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ilinunua eneo lote la Urafiki kwa bei ya Sh bilioni 3/-. Eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 50 linajumuisha nyumba, maghala (warehouses), viwanja, viwanda, pamoja na mali nyingine. Bei? Sh. bilioi 3/- sawa na jumba moja tu la kifahari liliko Mbezi Beach, au Mikocheni au Masaki!
NHC wameahidi kuboresha eneo hilo kuwa la kisasa zaidi kwa makazi na uwekezaji wa viwanda. Inawezekana NHC wana mpango kabambe wa kugeuza eneo hilo liwe na tija zaidi kuliko ilivyo sasa.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizi mpya za NHC za kutaka kubadili hali ya Urafiki, yapo maswali ya kimsingi sana ya kujiuliza. Kwamba ni kitu gani hasa kilizuia Urafiki kuendelea kuwapo na izalishe vema bidhaa za nguo? Kumekuwa na hoja inajengwa kwa nini Urafiki ilikufa kama ambavyo vilikufa viwanda vingine vingi vya nguo nchini. Kule Arusha kulikuwa na Kilitex, Mwanza kulikuwa na Mwatex, Musoma kulikuwa na Mutex na vingine vingi ambavyo navyo vimekufa kama ambavyo leo hii Urafiki imekufa na kuzikwa kabisa. Hoja hii inajengwa kwenye utetezi dhaifu sana kwamba tekinolojia ya viwanda hivi ilipitwa na wakati.
Ni kweli, tekinolojia za viwanda hivi ilipitwa na wakati, lakini tekinolojia mpya ilikuwapo, ipo na inaendelea kubuniwa. Swali la kujiuliza kwa nini haikuwezekana kubadili hata kiwanda kimoja kuingia kwenye tekinolojia ya kisasa katika kuzalisha bidhaa za nguo?
Katika maisha ya binadamu kuna mahitaji muhimu makuu matatu, chakula, mavazi na makazi. Kwa maana hiyo, hata itokee nini mahitaji ya nguo hayawezi kwisha kadri binadamu anavyoishi. Kinachobadilika ni mitindo tu, lakini mitindo yote hiyo ni nguo. Iwe iwavyo binadamu atahitaji mavazi.
Sasa katika mazingira hayo, inakuwaje leo tunaona fahari sana kila tunachovaa kama nguo kinatoka nje ya nchi? Nguo nyingi zinatengenezwa bara Asia kama Uchina, Vietnam, Malaysia na kwingineko. Viwanda vingi vya nguo vya Ulaya na Marekani vilihamishiwa Asia. Viwanda hivyo viko Asia, lakini soko lao liko Marekani na Ulaya. Maana yake ni kwamba hakuna mbadala wa nguo, hata kama wakikimbiza viwanda Ulaya au Marekani kwa sababu za gharama za uendeshaji, bado watalazimika kununua hizo nguo kwa gharama zao ijapokuwa wanaweka viwango wanavyotaka wao.
Ndiyo kusema kwamba ile tu kuachia viwanda kama Urafiki kufa na kuzikwa kabisa, kama ambavyo tulifanya kwa viwanda vingine vingi, huku tukishabikia mitumba kujaa nchini, ni kielelezo cha uvivu wa kutafuta suluhu ya matatizo yetu kama taifa. Nguo ni bidhaa inayokuza mnyororo wa thamani wa zao la pamba. Mkulima anayelima pamba atapata uhakika wa soko la mazao yake kwa kuwa nchini vipo viwanda vinavyozalisha nguo; vijana wa Kitanzania watapata ajira kwa sababu vipo viwanda vya nguo vinazalisha bidhaa bora; tutauza nje bidhaa bora za nguo kwa sababu tunazalisha ndani ya nchi; tutaingiza fedha za kigeni za uhakika kwa sababu tunazalisha kwa uhakika. Viwanda vya nguo vilisaidia kilimo, vilisaidia ajira, vilijenga uchumi imara.
Kwa sasa ukitaka kuitwa majina mabaya na wenye madaraka, waulize swali hili, ‘Ni nini hasa utatuzi wa ajira kwa vijana kwa malaki wanaoingia kwenye soko la ajira kutoka vyuoni kila mwaka?’ Hili siyo swali zuri. Halipendezi. Majibu ya watawala wetu yamekuwa kwamba vijana wajiajiri. Kujiajiri siyo kitu kibaya, ni jambo zuri. Hata hivyo, kudhani kwamba vijana wote watajiajiri ni kutokuwa wakweli jinsi shughuli za uchumi zinavyoendeshwa duniani kote. Watakuwapo wachache watakaojiajiri, lakini nao wataajiri wengine. Kwa maana hii jukumu la kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya vilivyokwisha kuwekezwa viendelee kustawi ni adhimu sana kwa ustawi wa taifa.
Tunakumbuka wakati wa mdororo wa uchumi wa mwaka 2009 serikali ya kibepari ya Marekani iliinusuru kampuni ya kutengeneza magari ya General Motors (GM) isifilisike kwa kuipa pesa. Ilikisiwa kuwa jumla ya Dola za Marekani bilioni 50 zilitolewa na serikali kuinusuru GM. Kisa? kufa kwa GM kungekuwa na athari mbaya zaidi kwa uchumi na watu wa Marekani.
Kama taifa ni lazima tuwe na mipango mikubwa, migumu na michungu wakati mwingine ili kujijenga kuwa imara. Rais John Magufuli aliposema angejenga reli ya kisasa ya SGR na kwamba treni zake zingekuwa za umeme, wapo watu walimwona anaota mchana. Hata aliposema atajenga daraja la Kigogo-Busisi kule Mwanza, pia alionekana anaota mchana. Vivyo hivyo, Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere. Uhakika ni kwamba taifa ambalo linajiruhusu kuondolewa katika njia ya maendeleo himilivu kwa sababu nyepesi kama za eti kubadilika kwa tekinolojia, limejitafutia kubakia katika utegemezi na ufukara mbaya. Hatuwezi kuwa taifa linalolima pamba halafu tunavaa kila kitu kutoka nje. Hatuwezi kuendelea kusimulia kwamba tulikuwa na Urafiki Textile, Mwatex, Kilitex, Mutex na vinginevyo, wakati mahitaji ya nguo kwa watu wetu leo ni makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya 1980 na 1990. Lipo soko kubwa la nguo, idadi ya watu wetu inakua kwa kasi kubwa sana, si ajabu kwamba sasa hivi tunanusa milioni 65 hivi. Ni wakati wa kuamua, maamuzi magumu, tujenge uwezo wa taifa kutengeneza ajira, kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo. Haya yanawezekana kwa kurudi pale tulipoanza na viwanda vya nguo. Hatujachelewa. Tunaweza kujirudi.