Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuridhishwa na upatikanaji wa bidhaa za vyakula na kuwataka wafanyabiashara kutopandisha bei wakati Ramadhani itakapoanza.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipotembelea Masoko ya Jumbi, Mwanakwerekwe na Darajani kuangalia mwenendo wa biashara na upatikanaji wa bidhaa za vyakula kuelekea mwezi wa Ramadhani.
Ameeleza kuwa Serikali inajipanga kwa ajili ya Ujenzi wa Masoko mengine maeneo mbalimbali ili kila mfanyabiashara afanye biashara kwenye mazingira rasmi .

Kuhusu usafi wa masoko ameuagiza uongozi wa masoko hayo kutafuta njia bora zaidi ya uhifadhi wa bidhaa za wafanyabiashara ili masoko kuwa safi wakati wote.
Amezielekeza taasisi zinazosimamia masoko hayo kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji na vipooza hewa katika masoko yote pamoja na kuimarisha usafi.
Ziara hiyo ya Rais Mwinyi ni ya kwanza tangu kufunguliwa kwa masoko mapya ya Jumbi , Mwanakwerekwe na ukarabati mkubwa wa Soko la Darajani.