YAPO mambo yanayotambulisha viwango vya maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla. Miongoni mwa hayo ni ubora wa miundombinu kama barabara, reli, viwanja vya ndege na huduma za kijamii kwa ujumla wake. Ukitembelea nchi yoyote bila hata kuelezwa kwamba imepiga hatua za maendeleo kwa kiwango gani, ile tu kuangalia majengo kama ya hosipitali na shule na huduma zinazotolewa humo, ni rahisi kutambua kama kuna hatua zimepigwa za maana au ni bado sana.
Miongoni mwa huduma muhimu kwa jamii yoyote ambayo inapambana kupiga hatua za maendeleo ni usafiri wa umma. Ukitembelea nchi yoyote duniani aina ya usafiri wa umma katika miji yake, itakupa picha halisi ya hatua zilizopigwa.
Unapokuwa na mfumo wa usafiri wa umma unaoeleweka, uliopangiliwa, unazingatia usalama na wenye kutabirika kwa maana kwamba ni wakati gani kwa uhakika huduma inapatikana, ni dhahiri taifa hilo kwa eneo hilo linakuwa limepiga hatua. Kinyume cha hali hii, maana yake bado taifa husika linapambana kujitafuta.
Tanzania kama yalivyo mataifa mengine duniani nayo ina maeneo katika huduma za kijamii imepiga hatua. Kwa mfano, huwezi kufumba macho ili usione na hivyo usitambue huduma bora kabisa inayotolewa na usafiri wa reli kwa sasa kupitia reli mpya ya SGR inayotoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Kukwepa au kukataa kutambua ubora wa huduma hii ambayo ilianza mwaka jana nchini, ni sawa na kukataa kutambua ukweli kwamba jua linang’aa.
Pamoja na hatua hizi katika usafiri wa umma kupitia reli, Tanzania kama taifa bado tunasumbuliwa na usimamizi wa sekta ya usafiri na usafirishaji. Kwa mfano, katika miji karibu yote huduma ya usafiri wa umma siyo ya uhakika na salama vya kutosha. Usafiri wa daladala katika miji yetu ni wa mashaka sana kwa maana ya usalama wa vyombo vinavyotumika. Ubora wake, nidhamu ya madereva na makondakta wao katika kuheshimu na kutii sheria za usalama barabarani ni changamoto kubwa.
Mgeni yeyote anayeingia nchini na kukutana na aina ya usafiri wa umma kwa kutumia daladala anapata picha ya wazi kwamba, hawa watu bado sana katika eneo hili.
Lakini mgeni akiangalia huduma ya usafiri wa umma ambayo katika miaka ya hivi karibuni serikali imehalalisha ya usafiri wa bodaboda na bajaji, anapata mashaka makubwa zaidi. Mashaka haya yanatokana na usalama wa vyombo hivi.
Ni hakika usafiri wa bodaboda ni janga kubwa la usalama barabarani nchini kwa sasa. Hili wala halihitaji uchunguzi wowote, ni dhahiri uendeshaji wa bodaboda katika miji yote ya Tanzania unafanana. Ni kama madereva wa bodaboda wameshindikana. Ni kama polisi kikosi cha usalama barabarani wamenyoosha mikono kwa hawa watu.
Ni nadra sana kumkuta dereva wa bodaboda akizingatia sheria, hata ile ambayo inamsaidia yeye binafsi kama vile kuvaa kofia ngumu, kuvaa makoti ya kujikinga na upepo, kuvaa viatu vya kulinda miguu yake au hata kuvaa miwani ya kukinga macho yake dhidi ya upepo mkali. Wanachofanya madereva wa bodaboda ni vurugu. Wanafanyiana vurugu wenyewe kwa wenyewe, lakini pia wanafanya vurugu kubwa dhidi ya vyombo vingine vya moto barabarani. Madereva wa bodaboda ni kama wamejitoa muhanga. Kwamba lolote litakalotokea dhidi yao katika vurugu za uendeshaji wa vyombo hivyo, kwao ni sawa tu.
Katika vurugu hizi, bodaboda badala ya kuwa mkombozi wa huduma ya usafiri wa umma, sasa zinakuwa janga. Kwa mfano wiki iliyopita Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo aliliambia Bunge kuwa jumla ya madereva wa bodaboda 759 walifariki dunia kutokana na ajali kati ya mwaka 2022 na 2024, huu ni wastani wa mareva 253 kwa mwaka. Hawa ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa. Aidha, ajali hizo zilisababisha vifo vya wananchi 283 katika kipindi hicho. Kwa maneno mengine ni kwamba kati ya mwaka 2022 na 2024 watu 1,042 walikufa kutokana na ajali za bodaboda. Hakuna maneno yanayotosha kueleza janga hili. Hii ni idadi kubwa mno ya vifo vinavyosababishwa tu na uzembe na kutokujali kwa madereva wa bodaboda.
Ukisikiliza visingizio vya askari wa kikosi cha usalama barabarani juu ya janga hili na ni kwa nini wameshindwa kuwadhibiti kabisa bodaboda, unapigwa butwaa. Eti bado wanaendelea kutoa elimu. Eti wanataka kushirikisha jamii itambua madhara ya kupanda bodaboda ambazo hazizingatii sheria za usalama barabarani. Yaani trafiki wetu kwa matendo halisi wanakiri kwamba wameshindwa kuwadhibiti madereva bodaboda.
Kwa mfano, inawezekana vipi bodaboda anapita kwenye taa nyekundu kwenye makutano ya barabara ambayo huongozwa kwa taa na trafiki yupo anaona, lakini asifanye chochote? Au inakuwaje trafiki anapishana barabarani na bodaboda iliyopakia mshikaki (abiria zaidi ya mmoja) bila kufanya lolote? Au inawezekana vipi trafiki anapishana na madereva wa bodaboda ambao hawajavaa chochote cha kujikinga kama ambavyo sheria inafafanua na hafanyi chochote? Hawavai kofia ngumu, hawavai viatu, hawavai miwani, hawavai makoti ya kuzuia upepo hawafanyi chochote kinachohusu usalama wao, wala wa chombo wanachoendesha wala usalama wa watumiaji wengine wa barabara. Trafiki wanaona na hawafanyi chochote!
Ni kweli bodaboda zimerahisisha usafiri wa umma. Ni kweli zimetatua changamoto ya usafiri hasa sehemu za vijijini ambako zamani ilikuwa kufika ni tabu. Hata hivyo, pamoja na nafuu hii kiwango cha vifo vinavyotokana na uzembe wa uendeshaji wa vyombo hivi ni jambo linalohitaji hatua madhubuti za kukabiliana nalo.
Kuna nyakati madereva wa bodaboda wanajiunga kama makundi ya wahalifu na kufanya vitendo vibaya vya uharibifu wa mali ikitokea mmoja wao amehusika kwenye ajali. Imetokea mara kadhaa madereva wa bodaboda kuitana ili kwenda kufanya uhalifu kwenye matukio ya ajali ambayo aghalabu huusisha vyombo vingine vya moto kama magari. Tumeshuhudia magari ya watu yakipopolewa mawe na hata mahali pengine kuchomwa moto. Vitendo hivi vinafanywa na madereva wa bodaboda kwa kile kinachoonekana ni kulipiza kisasi kwa mwenzao aliyehusika kwenye ajali. Kwa maneno mengine madereva wa bodaboda siyo tu wanavunja sheria kwa kutokuheshimu sheria za usalama barabarani, bali pia wanajichukulia sheria mkononi kwa kufanya vitendo vya kijinai vya kuharibu mali na hata kujeruhi watu.
Ukitafakari kwa kina sana utagundua kwamba kinachowadekeza hawa madereva wa bodaboda siyo trafiki tu, hata wanasiasa wanaamini kwamba utitiri wa bodaboda katika miji yetu ni ajira ya maana kwa vijana wa Kitanzania. Inawezekana kuwa ni ajira, lakini ukitafakari zaidi ajira hii siyo ya maana sana hata kama hawa watu jioni wanapeleka chakula nyumbani kwao na familia zinakula. Yapo madhara ya kiafya kwa uendeshaji wa bodaboda bila kuchukuwa hadhari.
Ingeliweza kuwa ni ajira ya maana kama, mosi, kungekuwa na utaratibu na udhibiti wa kutosha. Suala la usalama kwa madereva na abiria wao lisiwe na muhali. Kwamba iwe ni marufuku inayotekelezeka kwa dereva wa bodaboda kuendesha chombo hicho bila kuwa amekamilika. Yaani amevaa kofia ngumu pamoja na abiria wake; amevaa koti la kujikinga dhidi ya upepo; amevaa viatu vya kufunika miguu ili kujikinga dhidi ya madhara yoyote na azingatie sheria na alama zote za usalama barabarani.
Najua kuna watu watasema si rahisi kudhibiti bodaboda, wenye mashaka na hilo watembelee jiji la Kigali, Rwanda, halafu waje hapa waseme kama kuna dereva wa bodaboda anayeendesha pikipiki yake kama hajakamilika kwa viwango na vigezo vyote ya usalama. Hatuwezi kuendelea na hali hii ya kusababisha vifo vya watu kila uchao kisa eti madereva wa bodaboda hawadhibitiki kwa sheria tulizotunga sisi wenyewe na kukubali kuwa ndizo zitakazotuongoza ili tuwe salama tuwapo barabarani na vyombo vya moto.