Na Mwandishi Wetu
IDARA ya Uhamiaji Tanzania imetangaza majina ya vijana 331 waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya idara hiyo kuanzia Machi 1, 2025.
Tangazo la kuitwa kwenye mafunzo hayo limetolewa leo Alhamisi Februari 6, 2025 na Kamishna Jenerali wa idara hiyo.
“Kamishna Jenerali wa Uhamiaji anawatangazia vijana ambao wamechaguliwa kujiunga na Idara ya Uhamiaji kuripoti Chuo cha Uhamiaji cha Raphael Kubaga kilichopo Boma Kichakamiba, Wilaya ya Mkinga – Mkoani Tanga, Jumamosi Machi mosi 2025 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana,” imeeleza taarifa hiyo.

Pia, kwa walioomba na kuchaguliwa kupitia Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, wanatakiwa kuripoti Afisi ya Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja (Tunguu) Jumatatu Februari 24, 2025 saa 2:00 asubuhi.
Katika taarifa hiyo vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo wametakiwa kuripoti wakiwa na vyeti halisi vya elimu na fani mbalimbali.