Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Malawi, Lazarus Chakwera amemuagiza Kamanda wa Jeshi la nchi hiyo kujiandaa kuondoa Majeshi ya Malawi, kutoka eneo la Mashariki la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kulingana na taarifa Televisheni ya Serikali.
Taarifa hiyo ilisema uamuzi wa Rais unalenga kuheshimu tangazo la kusitisha mapigano kati ya pande zinazozana, ingawa uamuzi wa kusitisha mapigano ulikuwa ni mpango wa waasi wa M23, ambao uliibuka baada ya kundi hilo kushambulia Nyabibwe katika Jimbo la Kivu Kusini mwa DRC.

Rais Lazarus Chakwera alikuwa chini ya shinikizo la kuondoa Majeshi ya nchi yake Mashariki mwa DRC, baada ya wanajeshi watatu wa Malawi kuuawa katika mashambulizi ya M23 mjini Goma.
Wanajeshi hao walikuwa sehemu ya Ujumbe wa kulinda amani wa Kusini mwa Afrika uliotumwa na SADC kusaidia mamlaka ya Congo, kukabiliana na makundi yenye silaha katika eneo la mashariki linalokabiliwa na mzozo.