Katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Rashidi Kawawa eneo la Morocco yako majengo makubwa ambayo yamebadili mandhari ya jiji la Dar es Salaam, hususan sehemu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni.
Majengo haya kadhaa ndani ya eneo moja, yaliyoko mkabala na kituo cha daladala na kile cha mabasi yaendeayo haraka (mwendo kasi) Morocco, ni mali ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), chini ya mradi unaofahamika kwa jina la Morocco Square.
Mradi huu umekamikila kwa asilimia 100 na tayari majengo na sehemu kadhaa za mradi huo yameanza kupangishwa na nyingine kuuzwa. Taarifa ya NHC inasema maeneo ya maduka (Retail Mall) yamepangishwa kwa asilimia 100, wakati ofisi zikiwa zimepangishwa kwa asilimia 95.
Katika jengo lenye nyumba za makazi 100, tayari nyumba 85 zimeshauzwa na mauzo ya nyumba zilizobakia yanaendelea na upangishaji wa Hoteli yenye vyumba 81 umefanyika kwa asilimia 100 na hoteli hiyo imeanza kutoa huduma.
Morocco Square ni moja ya miradi mikubwa iliyoanza kukwamuliwa chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya Serikali kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukopa fedha kwa ajili ya kuikamilisha. Miradi hiyo mikubwa ilisiama kutekelezwa tangu mwaka 2018.

Mradi mwingine mkubwa ni ule wa Kawe 711, ambao umeshuhudia kurejea kwa mkandarasi Estim Construction Company Limited kuendeleza ujenzi wake tangu Januari 2024. Ujenzi huo unajumuisha nyumba 422 na sehemu za biashara, ukiwa na thamani ya Shilingi Bilioni 169. NHC wanasema ujenzi wake umefikia asilimia 50 na kwamba unatarajiwa kukamilika Aprili 2026.
Katika kuenzi jitihada za Rais Dkt Samia, NHC ilibuni mradi wa nyumba 5,000 wa Samia Housing Scheme zenye gharama ya shilingi bilioni 466. Mradi huo tayari umeanza kutekelezwa Kawe, Dar es Salaam, ambako zinajengwa nyumba 560 ambazo ujenzi wake umefikia asilimia 80, ukitarajiwa kukamilika Februari 2025.
“Mradi huu utawezesha ujenzi wa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini Mauzo ya nyumba 560 eneo la Kawe hizo yamekamilika na NHC inajiandaa kuanza awamu ya pili ya mradi huu eneo la Kawe nyumba 560 na Medeli Dodoma nyumba 100,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NHC.
Kadhalika utekelezaji wa mradi wa ‘Samia Housing Scheme’, unajumuisha ujenzi wa majengo ya kimkakati ya shughuli za Ofisi na biashara katika maeneo mbalimbali nchini ambayo ni Kahama mkoani Shinyanga, Masasi mkoani Mtwara, Mtanda mkoani Lindi na jengo la 2H (2H Commercial Building) mkoani Morogoro.
UJENZI WA MIRADI YA ‘SAMIA HOUSING SCHEME’
JINA LA MRADI | MKOA | HATUA YA UJENZI |
Kahama | Shinyanga | 70% |
Masasi Plaza | Mtwara | 40% |
2H Commercial Building | Morogoro | 40% |
Mtanda Commercial Building | Lindi | 30% |
Kadhalika NHC chini ya awamu ya uongozi wa Rais Samia, inajivunia kutekeleza majukumu ya usimamizi na ushauri elekezi wa miradi kadhaa ikiwamo ya ujenzi wa soko la Kariakoo wenye thamani ya Sh. bilioni 28 ambao umekamilika kwa wastani wa asilimia 97 na usanifu na usimamizi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango katika eneo la Mtumba, Dodoma ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 85 chini ya Kampuni ya Estim Construction.
Miradi mingine ni usimamizi wa ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira (Awamu ya Pili), ambao ujenzi wake umefikia asilimia 88 ukijengwa na Suma JKT na usanifu na ujenzi wa jengo la soko la madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara, kazi ambayo imekamilika na ujenzi kufikia asilimia 86.
HATUA ZA USANIFU NA USIMAMIZI WA MIRADI YA UJENZI
MRADI | KAZI | HATUA |
Soko la Kariakoo | Usimamizi wa ujenzi | 97% |
Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango | Usanifu na Usimamizi | 85% |
Ofisi ya M/ Rais – Mazingira (II) | Usimamizi wa ujenzi | 88% |
Jengo la soko la madini (Tanzanite) Mirerani, Manyara | Usanifu na ujenzi | 86% |
Miradi ya ukandarasi

Taarifa ya NHC inasema mafanikio mengine ambayo shirika hilo limepata kwa miaka minne iliyopita ni kuaminiwa kupewa ukandarasi wa miradi kadhaa ya kimkakati yenye thamani ya Sh. Bilioni 186, katika eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.
Baadhi ya miradi hiyo imekamilika, huku mingine ikiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji wake. Miongomi mwake ni ujenzi wa majengo ya Ofisi nane za Wizara mbalimbali ambao umefikia asilimia 90.
Miradi mingine iliyotekelezwa na NHC ni Ujenzi wa jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao umefikia asilimia 80 ukigharimu Sh. bilioni 9.7.
Miradi mingine ni ile inayogusa sekta ya Afya, ikihusisha Ujenzi wa Hospitali za Kanda ya Kusini (Mitengo), Hospitali ya Kanda ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Musoma (Mara) ambayo imekamilka na ukamilishaji wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete kwa asilimia 100.
“Miradi mingine ni ujenzi wa jengo la Ofisi pamoja na uzio wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Temeke Dar Es Salaam ambao umefikia asilimia 40 na ujenzi wa ghala la chakula la Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambao umekamilika kwa asilimia 100,” insoeka sehemu ya taarifa ya NHC na kuongeza:
“Shirika lilikamilisha pia ujenzi wa miradi 17 yenye majengo 44 ya Wakala wa Misitu Tanzania-TFS yenye thamani ya Sh. Bilioni 12.96, pia majengo mawili ikiwemo Ofisi na miundombinu kwa ajili ya tanuru (incinerator) la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ambayo imekamilika kwa asilimia 100 Jijini Dodoma na ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini Dodoma unaendelea na umefikia asilimia 34.”
Sera ya ubia
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) tayari limeingia katika kutekeleza ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma baada ya kuuhisha sera yake ya usimamizi ambayo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Novemba 16, 2022.
Mwaka 2024, NHC liliidhinisha na kusaini mikataba ya miradi 21 ya ubia yenye thamani ya Sh. 179 bilioni na kwa sasa miradi 18 iliyopata vibali vya ujenzi imeanza kutekelezwa, ikiwa kwenye hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 3 imeshapata vibali na hivi karibuni itaanza kutekelezwa.
Taarifa ya utendaji wa NHC kwa miaka minne iliyopita, inasema utekelezaji wa sera ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP), unahusisha miradi ya sasa na ile ya zamani ambayo ilikuwa imesimama katika maeneo mbalimbali nchini.
“Miradi minne iliyokuwa imesimama imesharejeshwa kwenye Shirika ili ikamilishwe na Shirika lenyewe. Lengo la Shirika ni kuhakikisha miradi yote ya ubia isiyokamilika inarejeshwa katika Shirika na mazungumzo na wabia wenye miradi hiyo yanaendelea,” inasema taarifa hiyo.
NHC inasema inaendelea na mchakato wa upembuzi na tathimini ya kina kwa waombaji wapya kwa miradi mingine kwenye maneneo kadhaa yanayohitaji kuendelezwa na kwamba sasa iko kwenye hatua ya kupata idhini kwa ajili ya kuendeleza viwanja hivyo visivyopungua 80 kwa nchi nzima.
Taarifa hiyo inasema kupitia PPP, NHC limeshirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara, huku ikitoa mfano wa eneo la Kariakoo ambalo lilikuwa na wapangaji 172 ambao nyumba zao zimevunjwa na kuendelezwa, na sasa zitapatikana nyumba zaidi ya 2,100 za makazi na biashara.
Lilikotoka NHC
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilianzishwa mwaka 1962 kwa Sheria ya Bunge Na. 45 kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora. Tangu kuanzishwa kwake, limekuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya nyumba nchini Tanzania.

Kuanzishwa kwake yalikuwa nimaono ya Rais wa kwanza, Mwl. Julius Nyerere kuhakikisha mahitaji ya msingi ya mwanadamu yanapatikana kwa urahisi. Mwanzoni kabisa, NHC lilitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya umma, lakini changamoto za kiuchumi na kisheria ziliathiri utendaji wake.
Mageuzi ya kihistoria yalifanyika kati ya 1990 na 2008 wakati sheria ambazo hazikuwa rafiki kuendeleza sekta ya nyumba zilipobadilishwa na NHC kupewa mamlaka mapya ya kujiendesha kibiashara bila kusahau jukumu lake la msingi. Hatua hizo ziliweka msingi wa kuboresha huduma za makazi kwa Watanzania, na chini ya uongozi wa Dkt. Samia kasi ya utekelezaji wa miradi ya nyumba imeongezeka.
Mwaka 2015, NHC lilianzisha Mpango Mkakati wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25), uliolenga kujenga nyumba 10,000 na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi. Katika kipindi cha Uongozi wa Dkt. Samia utekelezaji wa mpango huu umechukua sura mpya, ikiwemo uanzishaji wa miradi mikubwa kama “Samia Housing Scheme” ambayo inatarajiwa kuwa zitajengwa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mafanikio
Hadi sasa, NHC limefanikiwa Kujenga zaidi ya nyumba 30,000 za makazi tangu kuanzishwa kwake na linaendelea kujenga nyumba za kuuza na kupangishwa. Katika kipindi cha Awamu ya Sita, NHC limekamilisha miradi mikubwa, ukiwamo ujenzi wa nyumba 887 za makazi katika eneo la Iyumbu na Chamwino na Mtukula mkoani Kagera.
Pia kupitia mradi huo, nyumba nyingine mpya 68 ujenzi wake unaendelea katika eneo la Iyumbu na umefikia 90%. Kadhalika nyumba 521 za makazi na biashara zimejengwa katika maeneo ya Mtukula (Kagera), Medeli (Dodoma) na Dar es Salaam.
Katika kipindi cha miaka minne, shirika lilifanya ukarabati wa majengo katika mikoa mbalimbali, ambao ulijumuisha kupaka rangi na ujenzi wa mifumo ya maji taka.
“Tangu mwaka 2023 Shirika limekuwa likitenga Sh. bilioni 7 kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zake nchini kote. Hii imewezekana kutokana na kuimarika kwa uwekezaji na kuongezeka kwa mapato,” inasomeka sehemu ya taarifa ya NHC na kuongeza:
“Ankara za kodi ya nyumba zimepanda kutoka Sh. bilioni 7.5 mwaka 2021 hadi Sh. bilioni 9.4 hivi sasa, huku makusanyo ya kodi yakiwa zaidi ya asilimia 100. Kadhalika mwaka 2021 Shirika lilikuwa na maeneo yasiyopangishwa (vacancies) yanayofikia nyumba 700, na sasa maeneo hayo yameshapangishwa kwa asilimia 80, hii ikitokana na kuimarika kwa uchumi na biashara za Watanzania.”
Kwa upande wa madeni, NHC limefanikiwa kukusanya kiasi kikubwa ambapo miaka minne iliyopita Sh. bilioni 8.3 zimekusanywa, huku mauzo ya nyumba mpya yakiongezeka. Kwa mradi wa Kawe pekee, nyumba zote 560, zimeshauzwa kabla mradi kukamilika.
Kupitia ushirikiano na benki zaidi ya 22, NHC limewezesha wananchi kupata mikopo ya nyumba ya muda mrefu, huku sera ya ubia iliyohuishwa mwaka 2022 ikitajwa kufungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika miradi ya nyumba yenye thamani ya shilingi bilioni 191.
Thamani ya rasilimali
Hadi Juni 2024 kwa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), rasilimali za NHC zilikuwa zimefikia Sh. Trilioni 5.47, ikiwa ni 7.86% zaidi ya mwaka 2021 ambao zilikuwa Sh. Trilioni 5.04.
Ukuaji huo unatajwa kuchangiwa na kuongezeka kwa milki za Shirika kupitia nyumba mpya na umiliki wa maeneo mbalimbali ukiwamo ununuzi wa ardhi na majengo uliofanywa na NHC katika eneo la Urafiki, Dar es Salaam, ambayo awali yalikuwa yakimilikiwa na Kampuni ya Tanzania-China Friendship Textile Mills Co.
“Mnada wa kuuzwa eneo hili uliendeshwa na Kampuni ya Udalali ya Santana Investment Limited na NHC kufanikiwa kununua ekari 105 za ardhi katika viwanja vitatu vya kimkakati Jijini Dar es Salaam.
“Eneo lina unit 399 za makazi, majengo 6 ya biashara, makazi 32 ya wataalamu, Shule ya msingi, retail shop 32, maghala 31, yadi za magari 10, gereji 4, kituo cha mafuta kimoja, sehemu za kuoshea magari 3, fremu ndogo ndogo na makontena na Industrial Park,” insomeka taarifa ya NHC.
Miradi mipya
Taarifa ya NHC inasema Shirika hilo linaendelea kuweka mipango ya kuanzishwa kwa miradi mipya. Miongoni mwa miradi inayokaribia kuanza kutekelezwa ni Singida 2F uliopo Singida, Kashozi Business Center (Bukoba Mjini), Samia Housing Scheme Kawe Awamu ya 2 na Kijichi Jijini Dar es Salaam.
Mingine ni Mt. Meru Plaza eneo la Kibla Jijini Arusha, Juwata Plaza Morogoro, Medeli Awamu ya 3 Dodoma, Mkwakwani Plaza Tanga, Tabora Commercial Complex, Iringa ICC, Mpwapwa Flats Dodoma, Ilala Breweries Retail Shops na Mtwara Warehouse.
NHC linasema wanaedelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa ndani, ili kuwezesha uanzishaji wa miradi mipya ya makazi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, likiwamo na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), kutekeleza miradi ya ukandarasi, ujenzi wa vitega uchumi, kutoa ushauri wa kitaalamu kwa miradi mbalimbali nchini na kutekeleza sera ya ubia.
Kimsingi kwamiaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, NHC limepiga hatua kubwa katika kuboresha sekta ya nyumba nchini. Mafanikio hayo yanadhihirisha dhamira ya Serikali kuimarisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya makazi bora. Kwa mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa mwanga wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.