MWISHONI mwa wiki kulikuwa na taharuki kubwa kwenye mitandao ya kijamii kufuatia taarifa za kutekwa kwa Mwanaharakati Maria Sarungi, Mtanzania ambaye kwa kitambo sasa amekuwa akiendesha shughuli zake akiwa jijini Nairobi, Kenya. Hata hivyo, Maria alipatikana usiku wa Jumapili ya Januari 12, 2025 na kueleza kuwa hali yake ilikuwa njema. Katika picha mjongeo alionekana mwenye mashaka makubwa, na aliwashukuru wote waliopaza sauti baada ya taarifa za kutekwa kwake hivyo kufanikisha kuachiliwa huru. Aliahidi kueleza yaliyomsibu.
Siku moja baadaye Maria alieleza kuwa anashuku wahusika wa utekaji wake ni watu kutoka Tanzania. Maria amekuwa akiendesha midahalo na mijadala mingi katika mitandao ya kijamii, nyingi ikiwa inakosoa serikali ya Tanzania. Anaamini waliomteka ni watu wenye nasaba na serikali ya Tanzania, ingawa hajatoa uthibitisho wowote.
Nchini Kenya kama ilivyo Tanzania, yameripotiwa matukio mengi ya watu kutekwa. Kenya wimbi kubwa la utekaji wa watu liinaelezwa kuongezeka tangu Juni mwaka jana hasa baada ya maandamano ya Gen Z ambayo yalitikisa utawala wa Rais William Ruto.
Maandamano hayo yalikuwa yameitishwa kupinga muswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao raia wa Kenya waliutuhumu kuwa unakwenda kuongeza ugumu wa maisha kwao. Katika maandamano hayo; Bunge lilivamiwa na kuchomwa moto; maduka katika miji mbalimbali yaliporwa; na watu kadhaa waliuawa kwa kupigwa risasi za moto na askari. Hata hivyo, mwisho wa maandamano hayo Rais Ruto alilazimika kuuondoa muswada huo na kuvunja baraza la mawaziri.
Ingawa Gen Z walionekana kuwa wamepiga hatua kwa kuleta mabadiliko, kama vila kumfanya Rais alazimike kuuondoa muswada wa fedha wa mwaka 2024, na pia kuvunja baraza la mawaziri, matukio ya utekaji na kupotezwa kwa watu yanaibua maswali mapya juu ya utawala wa Rais Ruto.
Kwa mfano, hoja imekuwa kwamba je, Ruto aliwabururia Gen Z kamba ndefu ili wadhanie kwamba wamefanikiwa katika maandamano yao, na sasa anajibu mapigo kwa kumfuata mtu mmoja mmoja katika mfululizo wa matukio ya utekaji yanayoendelea nchini huko kwa sasa?
Picha ya kinachoendelea nchini Kenya ndiyo sura halisi ya nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwamba kiongozi mkongwe wa upinzani Dk. Kiiza Besigye alitekwa akiwa nchini Kenya na kurejeshwa kwao Uganda ambako sasa anakabiliwa na mashitaka, ni tukio ambalo wengi walitarajia kwamba lingemtokea pia Maria, lakini bahati njema ikawa kwake (Maria) hakuondoshwa Kenya.
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimesaini mkataba wa Jumuiya hiyo unaozishurutisha pamoja na mambo mengine, kulinda na kuheshimu haki za binadamu na utawala bora. Kwa mfano, Kifungu cha sita (d) cha mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unazitaka nchi wanachama wa Jumuiya kuongozwa kwa kanuni za utawala bora ikiwa ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala wa kidemokrasia, utawala wa sheria, uwajibikaji, haki za jamii, fursa sawa kwa wote, usawa wa kijinsia na uzingatiaji na ulinzi wa haki za binadamu kama zilivyokubalika katika Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.
Matukio ya utekaji wa raia katika nchi wanachama, siyo tu kwamba ni ukiukaji wa mkataba wa Jumuiya, bali pia ni uvunjaji wa sheria za ndani za nchi wanachama kwani nchi hizo zinaongozwa kwa katiba ambazo zimeainisha wazi mifumo ya kisheria ya kufuatwa katika kuendesha mashauri.
Pia, utaratibu wa kuteka watu ndani ya nchi moja mwanachama na kumpeleka nchi nyingine kwa sababu zozote zile, ni uvunjaji wa haki za watu chini ya kanuni za kimataifa za kutafuta hifadhi kwa kukimbia mateso au tishio dhidi ya maisha yao. Kwa maana hiyo, iwe ni serikali ilituma watu kuteka Maria na Besige, au ni watu walijituma wenyewe, kwa vyovyote siyo vitu vinavyostahili kuungwa mkono. Ziko sababu nyingi za kukataa utaratibu huo, mosi, mfumo wa sheria za nchi na mikataba ya kikanda na kimataifa, vinatoa utaratibu unaopaswa kufuatwa kama serikali moja inamuhitaji mtu wanayeamini ana mashitaka ya kujibu katika nchi zao.
Pili, utaratibu wa kuingia katika nchi moja na kuanza kuwasaka ili kuwateka wale wanaodhaniwa kuwa ni wakosoaji wa watawala, haukubaliki kisheria na kitaratibu. Matendo hayo ni uovu kama ulivyo uovu mwingine wowote.
Tatu, ni katika kutambua matukio haya ya kuzidi kuongezaka kwa matukio ya utekaji wa raia ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mtu anapaswa kujiuliza hivi Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ‘kitabu’ tu ambacho wala hakina maana yoyote? Je, watawala wetu katika nchi hizi ndani ya miaka ya hivi karibuni wameingiwa na hofu gani kiasi cha kuamua ‘kuruhusu’ makundi ya watu kuendesha matendo ya utekaji kana kwamba mifumo ya utawala wa sheria haifanyi tena kazi?
Juzi nchini Kenya kiongozi mmoja mkubwa alipiga kelele baada ya kutekwa kwa mwanaye. Amepiga kelele kubwa sana. Ni haki yake kwa kweli kumlilia mwanaye, ni haki pia kuungana naye kupaza sauti na pia kulaani matendo ya utekaji. Kuungana naye kulaani na kukemea utekaji ni jambo la kiungwana, kizalendo na ni moyo wa kuwasha na kusukuma mbele moto wa kutaka uzingatiaji wa utawala wa sheria katika nchi hizi.
Hata hivyo, yafaa kujiuliza wale wenye nafasi, uwezo na madaraka katika ngazi mbalimbali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, watakaa pembeni mpaka lini wakati matendo ya uhalifu ya utekaji watu yakizidi kuongezeka kila uchao? Watakaa pembeni kwa sababu hakuna wa nyumbani kwao ametekwa au kuuawa?
Ni rai yangu kwa kila Mtanzania, Mkenya, Mganda, Mnyarwanda, Mrundi, Mkongomani, Sudan ya Kusini na Msomali kupaza sauti katika ukubwa wa Jumuiya hii kukataa matendo ya kuteka raia kwa sababu yoyote ile. Iwe ni ajenda ya kudumu kuwaambia viongozi wetu, kuwaambia watawala wetu, kwamba utekaji ni hulka ya mkoloni. Utekaji ni hulka ya mdhalimu. Utekaji ni hulka ya mtu asiyejiamini na ambaye hana hoja. Serikali hizi zimechaguliwa na watu/wananchi, ni lazima ziwalinde wananchi. Tuwasukume watawala wetu na vyombo vilivyoundwa kulinda raia na mali zao kufuata sheria; vyombo vilivyoundwa kusimamia haki kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria ili raia katika nchi zetu wawe huru kweli.
Tujihami sasa kwa kupaza sauti wakati watekaji wakiwa kwa jirani kabla hawajaingia katika maboma yetu. Tusisubiri kuwalilia vijana na mabinti wetu wa kuzaa, tuungane kulia na majirani ambao watoto wao wametekwa na kupotezwa. Hiki ni kilio cha taifa, siyo cha mtu mmoja. Watu werevu hujifunza kwa makosa ya watu wengine, tujihami wote kwa kusema utekaji huu katika taifa letu sasa basi! Yatosha!