Na Safina Sarwatt, Moshi
Zaidi ya wanafunzi 1,000 kutoka familia zenye mazingira duni wamefaidika na mpango wa ufadhili wa masomo ulioanzishwa na Kiwanda cha Sukari TPC Moshi kupitia taasisi yake ya Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK). Mpango huu, ulioanza mwaka 2012, umewezesha wanafunzi wa maeneo yanayozunguka kiwanda hicho kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu.
Kwa mujibu wa Lazaro Urio, Msimamizi wa FTK, kiwanda cha TPC hutenga zaidi ya shilingi milioni 400 kila mwaka kufadhili wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kwenda vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 250 hunufaika kila mwaka kupitia mpango huu wa kipekee, ambao unalenga kupunguza changamoto za kifedha zinazozuia wanafunzi kuendelea na masomo.
“Mpango huu ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) wa TPC, ambapo tunalenga kubadilisha maisha ya wanafunzi na kupunguza pengo la kielimu katika jamii,” alisema Urio.
Miundombinu ya kisasa na ufadhili wa wanafunzi
Mbali na ufadhili wa elimu, FTK pia imewekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa maeneo yanayozunguka kiwanda. Hivi karibuni, taasisi hiyo ilikamilisha ujenzi wa bweni jipya lenye uwezo wa kuhifadhi wanafunzi 68 wa kike katika shule ya sekondari ya TPC.
Urio alieleza kuwa bweni hilo lilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 147, huku shule ikibeba jukumu la kununua vitanda. Ujenzi huu ulitokana na changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa kilometa 14 hadi 20 kwenda na kurudi shuleni kila siku.
“Changamoto ya umbali iliwafanya wanafunzi, hususan wa kike, kuchelewa kufika shuleni na kukosa vipindi muhimu. Uwekezaji huu unatoa fursa kwao kujikita zaidi katika masomo,” alisema Urio.
Kwa kuongezea, shule hiyo imepata maktaba ya kisasa yenye maabara ya kompyuta, iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 126. Maktaba hiyo inaweza kuhudumia wanafunzi 48 kwa wakati mmoja, lakini bado inahitaji shilingi milioni 25 kwa ajili ya kukamilisha mahitaji ya thamani.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana nasi katika kuhakikisha maktaba hii inapata vifaa muhimu vitakavyowezesha wanafunzi kupata elimu bora zaidi,” alisema Urio.
Manufaa kwa jamii
Kwa ujumla, TPC hutenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kila mwaka kupitia FTK kuhudumia wakazi wa maeneo ya Moshi Vijijini na wilaya ya Simanjiro, Manyara. Huduma hizi zinajumuisha si tu elimu, bali pia miradi mingine ya kijamii inayolenga kuboresha maisha ya zaidi ya watu 95,000 katika maeneo haya.
Huduma hizi ni mfano bora wa jinsi sekta binafsi inaweza kuchangia maendeleo ya kijamii kwa kuwekeza katika elimu. Kupitia ufadhili na uboreshaji wa miundombinu, TPC inachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuwasaidia vijana kufanikisha ndoto zao za kitaaluma.
Wanafunzi Wanufaika Wasimulia
Moja ya wanafunzi walionufaika, Gladines Kimaro, alieleza jinsi mpango huu umebadilisha maisha yao.
“Kabla ya bweni, tulilazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, hali iliyokuwa inachosha na kutufanya tukose vipindi. Leo hii tuna nafasi ya kujifunza kwa utulivu na kufikia malengo yetu,” alisema Kimaro.
Urio aliongeza kuwa mpango huu umechangia kupunguza utoro, hususan kwa watoto wa kike ambao mara nyingi walikumbana na vishawishi njiani.
Mpango wa TPC Moshi kupitia FTK unaendelea kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa familia duni katika maeneo ya Moshi na Simanjiro. Kupitia ufadhili wa masomo na uwekezaji katika miundombinu ya elimu, taasisi hiyo si tu inainua viwango vya elimu, bali pia inachangia mustakabali bora wa jamii kwa ujumla.
Hii ni hatua inayopaswa kuigwa na mashirika mengine, ikithibitisha kuwa sekta binafsi inaweza kuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya kijamii.