SGR imejibu, kuna jambo la kufanya Kituo Kikuu Dar

MIONGONI mwa miradi ya miundombinu ambayo imekuwa kwenye mijadala mingi ndani ya jamii ni ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway -SGR). Mradi huu ulikuwa ni ndoto ya nchi, lakini sasa hivi ni halisi. Kipande cha Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma, kimekamilika, na safari za treni zimekwisha kuanza. Safari kati ya Dar na Morogoro zilianza Juni 14 mwaka huu na safari kati ya Dar na Dodoma zilianza Julai 25 mwaka huu.

Kuanza kwa huduma ya usafiri wa treni ya SGR ambayo inatumia umeme, imeamsha ari kubwa na shauku ya watu wengi kutaka kutumia usafiri huo. Nia hasa ni watu kutaka kuwa mashuhuda kwamba usafiri huo kweli unafanya kazi na siyo ndoto tena kama ilivyokuwa awali.

Itakumbukwa kwamba wakati uzinduzi wa safari za treni hii unafanyika, watu wa aina mbalimbali walialikwa kusafiri nayo ili kuwa mashuhuda wa huduma hiyo ambayo ni kwa mara ya kwanza inapatikana nchini kwetu. Treni hii kwa kupindi hiki kifupi ambacho imekuwa inatoa huduma, imeteka watu wengi ambao sasa wanakimbilia kusafiri nayo kuanzia Dar kwenda Morogoro na hatimaye Dodoma.

Binafsi hivi karibuni nilipata fursa ya kusafiri na treni hii kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na kurudi. Ninashuhudia kuwa ilikuwa safari nzuri, yenye utulivu mkubwa, iliyozingatia ratiba ya kuondoka kama ilivyooneshwa kwenye tikiti ya abiria. Mwendo wa treni husika ulikuwa mzuri, kati ya Dar na Dodoma tulitumia saa tatu na ushei.

Wahudumu wa kwenye treni ni wasikivu, wanajituma kufanya kazi yao kwa juhudi kubwa, wanavaa nadhifu mavazi ya heshima, wanatumia lugha nzuri na kuhudumia bila kinyongo. Nakumbuka tukio moja la abiria jirani yangu aliamua kujilipua kwa vinywaji, alikuwa anaagiza kama ndiyo mwisho wa kunywa. Alikuwa anaita kila wakati, muhudumu alimsikiliza kwa heshima na utulivu na kumuhudumia kile alichokuwa anataka na kwa wakati. Nilifurahishwa na huduma kwa ujumla.

Kuhusu utulivu wa treni (stability) niliona ikiwa imetulia kweli kweli, viti vya kukalia abiria ingawa vinatofautiana kati ya daraja moja na jingine, vinampa abiria kukaa kwa starehe kabisa, abiria ana hiari ya kulaza au kusimamisha kiti chake kadri anavyoona inafaa kwa ukaaji wake. Usafi wa mabahewa kwa ujumla ni wa kiwango cha juu kama vilivyo vituo vya treni pia.

Kwa mtu aliyepata fursa ya kutumia huduma za treni katika nchi zilizoendelea kama Ulaya au Marekani au Japan, atakubaliana nami kwamba viwango vya treni hii ni sawa na hizo treni za huko majuu. Kuna nyakati mtu akiwa ndani ya treni hii anaweza kujisahau kwamba yuko Tanzania ambayo tulizoea ile treni ya zamani, yenye mwendo mdogo, kelele nyingi, mabehewa yaliyochakaa na huduma za kiwango cha chini kabisa. Aidha, mtu anaweza kudhani kwa anachokiona ni ndoto kwamba huduma kama hiyo inaweza kupatikana Tanzania tena kwa viwango hivyo.

Ni hakika, huduma hii imeanza na mguu mzuri. Abiria ni wengi, ukichelewa kukata tikiti ukasubiri dakika za majeruhi, ni dhahiri hutaipata. Nilishuhudia karibia kila kiti kikiwa na abiria, kwa maana hiyo uhitaji wa huduma hii ni mkubwa sana. Kuna rafiki yangu mmoja ni kati ya wafanyakazi wa serikali waliohamishiwa Dodoma baada ya uamuzi wa serikali wa kuhamia Dodoma, aliniambia kwa zaidi ya miaka sita amekuwa akisafiri kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam inakoishi familia yake kwa kutumia usafiri wa basi au mara nyingine kuendesha gari lake na wakati mwingine hali ya mfuko ikiwa nzuri hupanda ndege. Alishuhudia kwamba ametumia muda mrefu na gharama nyingi kwa safari hizo, lakini sasa anaona kama ukombozi umemfikia kukabiliana na hali hiyo kutokana na huduma ya treni ya SGR. Siku hizi anasafiri na treni ya Ijumaa jioni na kurejea Dodoma Jumapili jioni. Anafurahia huduma hiyo kwa kuwa imemuondolea shinikizo la safari ya zaidi ya saa nane Dar – Dodoma.

Kwa mwamko wa watu kutumia treni ya SGR itakuwa ni jambo lisilotarajiwa kwamba ubora wa huduma hii utaporomoka hapo ulipo sasa. Kikubwa ambacho wananchi wanatarajia ni kuongeza idadi ya safari kwa siku, kutoka mbili hadi tatu na kuendelea. Hakika Watanzania hawataki kuona ya Mwendokasi yakijirudia SGR. Gharama ya Sh. trillion 10.69 kujenga SGR kutoka Dar – Mwanza si haba, ni fedha nyingi. Ni lazima SGR itunzwe na kulindwa kama mboni ya jicho. Ni ukombozi wa taifa, kwa huduma na uchumi.

Wapo watu wamekwisha kuanza kulalamika kwamba biashara ya mabasi kati ya Dar – Moro- Dodoma kwa baadhi ya kampuni, imedoda. Mabasi mengi sasa hayana abiria, na kampuni hizo zimelazimika kupunguza idadi ya mabasi yao katika ruti ya Dar – Moro – Dodoma. Ni ukweli mchungu mtu kupoteza biashara ambayo ameimiliki kwa miaka na miaka, hata hivyo ni vema ikaeleweka kuwa zama zinabadilika. Maendeleo ya tekinolojia yanaleta fursa mpya na kuwasukuma pembeni wengine waliodumu katika mfumo na tekinolojia ya zamani. Hawa wajipange kivingine, waekekeze mabasi yao kwingine. Tanzania ni nchi kubwa, na huduma ya mabasi inahitajika kwingineko, si lazima Dar – Moro – Dodoma.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya ya kupigiwa mfano kuhusu treni ya SGR, kuna tatizo ambalo inabidi kufanyiwa kazi mapema. Kituo Kikuu cha SGR Dar es Salaam ni miongoni mwa vituo bora kabisa vya kuhudumia abiria. Kimejengwa vizuri, kinapendeza. Pamoja na umaridadi wote huu ukubwa wa kituo hiki katika siku chache zijazo wakati ujenzi SGR kuelekea Mwanza utakapokamilika, kutatokea changamoto ya kuhimili wingi wa abiria.

Ukitafakari treni hii itakapokuwa sasa inakwenda hadi Mwanza na Kigoma, idadi ya abiria pale kituoni itakuwa kiasi gani? Ni dhahiri ukubwa wa kituo haukuzingatia kwa makini wingi wa abiria watakaokuwa wanatumia kituo hicho muda mfupi ujao kuanzia sasa.

Kadhalika, ili abiria wafike kwenye kituo hiki kikubwa wengine wanalazimika kufika kwa magari yao, kuna msongamano mkubwa sana wa magari eneo la Barabara ya Sokoine mkabala na kituo hiki. Kuna vurugu mechi kubwa. Vurugu hizi ni nyingi wakati hata kituo cha Mwendokasi kilichoko mkabala na kituo hiki kikuu hakijaanza kazi. Ni jambo la kujiuliza kwa haraka kwa sasa, je, miundombinu hii itatosheleza na kuhimili idadi ya abiria wa treni ya SGR wakati sasa Kigoma na Mwanza watakuwa wanahudumiwa na treni hii. Pengine ni vema wataalam wakaanza kukuna vichwa kwamba hali pale stesheni inahitaji utatuzi wa haraka wa kisayansi ili kuondoa msongamano.

spot_img

Latest articles

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...

NECTA yawaonya wamiliki na wakuu wa shule

Na Winfrida Mtoi Baraza la Mtihani la Tanzania (NECTA), limewataka wamiliki na wakuu wa shule...

More like this

Tulia alipoteza fursa ya kuokolewa uhai wa Kibao

INAWEZEKANA Agosti 27 2024 ilikuwa ni siku ambayo maisha ya Ally Mohamed Kibao yangeokolewa...

DCEA yakamata kilo 1,815 za skanka

Na Mwandishi Wetu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata...

Waziri Mkuu: Suala la mazingira liwe ajenda ya Kitaifa

Na Mwandishi Wetu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe...