Na Winfrida Mtoi
Kocha wa zamani wa Simba, Patrick Aussems maarufu Ucheba, ametaja sababu ya kurejea kufundisha soka nchini kuwa ni kuvutiwa na mipango ya Singida Black Stars ambayo amejiunga nayo kwa sasa.
Uchebe ambaye aliipa Simba mafanikio makubwa akichukua mataji mawili ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, amewasili nchini jana Julai Mosi, 2024 na leo kuzungumza na waandishi wa habari kueleza mikakati yake.
Kocha huyo ameeleza kuwa pamoja na kupata ofa nyingi alizikataa baada ya kupigiwa simu na bosi Singida Black Stars na kumueleza mipango yao, huku akiahidi kuipaisha timu hiyo hadi kufikia mafanikio kama alivyofanya Simba.
“Unapoitaja Tanzania Ulaya watu wanaijua Simba zaidi. Ikumbukwe wakati naichukua Simba haikuwa katika hali nzuri lakini niliitengeneza ikawa timu bora yenye mafanikio, hivyo ndicho kitu ninachotaka kukifanya Singida na malengo kwa msimu wa 2024/2025 ni kumaliza nafasi ya tatu,” amesema Uchebe.
Kwa upande Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu hiyo, Jonathan Kasano, amesema wana malengo ya muda mrefu na mfupi na ndani ya miaka mitatu wanataka kuwa timu ya ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema wameshafanya usajili kwa asilimia kubwa na walimshirikisha kocha huyo, hivyo ni imani yao watafikia malengo wanahitaji kupitia kocha huyo ambaye ni mzoefu wa kufundisha timu mbalimbali.