Nairobi, Kenya
Rais wa Kenya, William Ruto, amekataa kutia saini na ameondoa kabisa muswada wenye utata wa fedha wa mwaka 2024, ambao umesababisha maandamano na vurugu nchini kote. Rais Ruto ametoa hotuba hiyo leo Juni 26,2024 kwa taifa baada ya maandamano makubwa yaliyofanyika nchini Kenya, hasa yakiongozwa na vijana waliolalamikia nyongeza mpya za ushuru wakisema zitawaongezea mzigo wa maisha.
Taarifa hii imekuja wakati waandamanaji wakiapa kuendelea na maandamano yao kupinga nyongeza hizo za ushuru, siku moja tu baada ya polisi kufyatua risasi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 20 katika maandamano hayo yaliyogeuka kuwa vurugu.
Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetangula, amewasifu vijana kwa ujasiri wao, lakini amesisitiza kwamba malalamiko yao lazima yafuate mkondo wa sheria ili yapate kusikilizwa.
Katika hali nyingine, mahakama ya Eldoret imesitisha operesheni zake kwa muda baada ya waandamanaji kuharibu hati muhimu hapo jana.