Aibu ya kufunga Jangwani, mpaka lini?

KATIKA miezi ya hivi karibuni, kuanzia mwishoni mwa mwaka jana na mapema mwaka huu, taifa letu limepata ‘neema’ ya mvua kubwa. Mvua hii ambayo aghalabu ni baraka, kutokana na kuhitajika sana na wakulima wetu wanaoendesha shughuli zao kwa kutegemea, imetuacha na majeraha mengi.

Katika maeneo mengi nchini mvua hii ilikuwa ni kubwa kupita kiasi, hasa ile ya mwaka jana ya El Nino na hata ya masika ambayo imeleta madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. Imeharibu miundombinu ya barabara na madaraja mengi nchini.

Mamia ya watu wamepoteza maisha yao, huku maelfu ya wakizihama nyumba zao baada ya kuzingirwa na mafuriko. Wapo wengi ambao kwa sasa wamepata hifadhi katika maeneo ya umma, huku wengine wakihifadhiwa na jamaa zao.

Ni vigumu kumlaumu yeyote kwa wingi wa mvua zilizonyesha, aidha ni muhali pia kulaumu yeyote kwa mafuriko yaliyotokea. Kwa mfano, ni jambo ambalo siyo la kiungwana kulaumu wale wakazi wa Hanang’ ambao walipatwa na janga la mmomonyoko mkubwa wa ardhi uliokuwa na tope baada ya mlima kumeguka. Kadhalika, ni kushindwa kutambua makali ya ongezeko la mvua za mwaka jana na mwaka huu kwa kuwalaumu watu wa mikoa ya Pwani hasa katika bonde la mto Rufiji, katika eneo la Kibiti wilayani Rufiji. Pia kuwalaumu wakazi wa maeneo ya Mbeya ambako mlima pia ulimeguka, nako ni kushindwa kutambua makali ya mvua za wakati huu na madhara yake.

Ni halali na haki kuwapa pole wote waliofikwa na maafa haya. Hawakupanga kuwa manusura au hata kupoteza ndugu na wapendwa wao katika janga hili. Tumesikia serikali ikisema kuwa itahakikisha miundombinu yote iliyoharibika, kuwa itakarabatiwa na kurejesha njia za mawasiliano kama zilivyokuwa hapo kabla. Ni jambo jema. Ni hekima na busara kuamini kwamba serikali itakwenda kufanya jambo hilo kwa ukamilifu wake.

Wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, alionekana akiwa amepiga kambi mkoani Lindi, kusisimamia kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Wananchi wa mikoa hiyo, hapana shaka, wamefarijika kuona walau kwa hatua za awali daraja lililozolewa na maji, juhudi zimefanyika na sasa magari yanapita. Hata hivyo, kazi kubwa ya kujenga daraja la uhakika mahali hapo bado haijaanza. Ni imani ya wananchi wengi kuwa daraja jipya litajengwa.

Pamoja na changamoto zote hizi za mafuriko, mvua kubwa, kimbunga na kila aina ya janga la asili lililotokea, bado akili za wakazi wengi wa Jiji kubwa kuliko yote nchini Tanzania, Dar es Salaam, wangali wanajiuliza maswali magumu kuhusu hali ya barabara kuu ya Morogoro eneo la Jangwani.

Miaka na miaka sasa serikali inajua, na inaelewa fika kwamba mfumo wa ujenzi wa barabara ya Morogoro eneo la Jangwani, hauhimili tena hali ya mafuriko yanayotokea katika jiji hilo katika mto Msimbazi.

Kwa mfano, miaka michache iliyopita Shirika la Mabasi ya Mwendo Kasi (DART) ilipata hasara kubwa ya kuharibika mabasi yake mengi ambayo yalikuwa yameegeshwa kwenye yadi yake ya Jangwani. Ingawa hadi sasa idadi ya mabasi yaliyoharibika haijawahi kuwekwa wazi, kuna taarifa kwamba ni zaidi ya mabasi 70 yaliharibika baada ya kujaa maji machafu ya mafuriko ya mto Msimbazi katika eneo la Jangwani.

Hadi leo, hakuna yeyote ambaye amepata kusema ilikuwaje wahandisi wa kizazi cha sasa chenye nyezo za kisasa bora kabisa za kung’amua hali ya eneo linalotaka kujengwa nyumba, au barabara au reli au ujenzi wowote, walishindwa kuelewa kuwa Jangwani kwa vyovyote vile pasingefaa kuwekwa yadi hiyo, kwa mfumo wa ujenzi uliofanyika pale? Ni nani hasa alipata kuwajibishwa kwa uzembe ule ambao ni moja ya sababu za kuyumba kwa huduma ya mabasi ya DART kutokana na kuharibika kwa idadi kubwa ya mabasi yake katika kipindi cha muda mfupi?

Lakini linalosumbua akili za wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni hili la kuona Jangwani pakigeuka kuwa sehemu isiyopitika, hata pale zinaponyesha mvua kidogo tu ambazo zinajaza mto Msimbazi. Je, pamoja na nchi hii katika miaka yake 61 ya uhuru na utitiri wa wahandisi wa ujenzi (civil engineers) waliyozalishwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini mpaja sasa, amekosekana hata mmoja wa kuiambia serikali kuwa Jangwani ni aibu ya kitaaluma kwa wahandisi wa nchi hii? Lakini pia ni fedheha kwa serikali kwa mji wake mkubwa wa kibiashara kukumbwa na kadhia ya kufungwa kwa barabara ya Morogoro eneo la Jangwani mwaka baada ya mwaka.

Kuna jambo jingine ambalo halisemwi sana pale Jangwani. Hivi yale magreda yaliyopiga kambi pale Jangwani mwaka mzima, ni ya nani? Je, yanalipiwa kiasi gani kwa kazi ya kuondoa tope na mchanga kila mto unapofurika? Nani ananufaika na mradi huu wa Jangwani kufurika kila wakati? Ni kwa nini hasa umma haujaona uharaka wa serikali wa kutaka kubadili hali ya barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kwa kufanya jambo la kiuandisi wa kisasa kwa kuinyanyua ili kuepuka maji kupita juu ya barabara? Ni hakika, wahandisi wa nchi hii wametembea maeneo mengi sana katika dunia hii. Wamejionea wenzetu walivyokabiliana na kero nyepesi kama za Jangwani kwa kubuni mfumo wa barabara na daraja rafiki kabisa katika eneo kama hilo. Hali kadhalika, viongozi wetu mbalimbali wamepata fursa ya kutembea maeneo mbalimbali ya dunia hii. Wameona na kujifunza mengi kwenye nchi zenye hali ya mito na ardhi oevu yenye changamoto kubwa kuliko hata Jangwani. Wameona jinsi wenzetu walivyokabili hali hiyo, ni nini hasa kinashindikana Jangwani? Utashi, fedha au miradi ya watu itakufa?

Kuendelea kuwa na hali ilivyo ya barabara ya Morogoro katika eneo la Jangwani ni fedheha. Ni aibu ya taifa, ni jambo ambalo linashusha sana hadhi na thamani ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati tukitafakari ukweli huu wa Jangwani, kila tunaposafiri ndani ya nchi, kwenye barabara mpya za lami na hata zile za changarawe, kuna jambo moja kubwa la muhimu la kiuhandisi limekuwa halipewi kipaumbele kwenye ujenzi wa barabara zetu. Suala la uwekaji wa mitaro ya kuchukua maji ya mvua pembezoni mwa barabara imekuwa kama ni hiari. Siyo jambo la lazima la kiuhandisi la kujenga barabara imara ambazo zitadumu kwa muda mrefu.

Ndiyo maana mvua zikinyesha kidogo tu, barabara zetu zinageuka kuwa mito. Kwa kanuni za kiuhandisi, barabara isiyokuwa na mitaro, haiwezi kuhimili mvua kubwa, na kwa maana hiyo hazitadumu. Kujenga barabara bila mitaro ni hujuma ya wazi kwa taifa. Ifike mahali tuseme sasa basi. Tondoleeni aibu ya Jangwani.

spot_img

Latest articles

Balozi Nchimbi awafariji Mzee Makamba na Familia ya Mwambi

Na Mwandishi Wetu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amemtembelea...

Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Dunia

Na Mwandishi Maalum, Washington D.C Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dk. Zarau  Kibwe, kuwa Mkurugenzi...

Shamba darasa kutoka Kenya: Hata Rais anatokwa jasho

KUNA kitu kinaitwa ‘shamba darasa’. Hili ni shamba ambalo huandaliwa na kuendeshwa kwa nia...

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

More like this

Balozi Nchimbi awafariji Mzee Makamba na Familia ya Mwambi

Na Mwandishi Wetu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amemtembelea...

Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Dunia

Na Mwandishi Maalum, Washington D.C Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dk. Zarau  Kibwe, kuwa Mkurugenzi...

Shamba darasa kutoka Kenya: Hata Rais anatokwa jasho

KUNA kitu kinaitwa ‘shamba darasa’. Hili ni shamba ambalo huandaliwa na kuendeshwa kwa nia...