‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 4,2024 Ikulu jijini Dar es Salaam, wiki hii waliripoti kwenye vituo vyao vya kazi. Miongoni mwa waliofika kwenye vituo vyao vya kazi na makabidhiano ya ofisi kufanyika ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ambaye Jumapili ya Aprili 7, 2024 alikabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Amos Makalla ambaye sasa ni Katibu wa CCM wa Itikadi na Uenezi.

Jumatatu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alimkabidhi ofisi Mkuu mpya wa mkoa huo, Paul Makonda. Mongela aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, huku Makonda akiondolewa kwenye nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM. Hadi Jumatatu wiki hii, Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi alikuwa bado hawajakabidhiana ofisi na mtangulizi wake, Mtanda aliyehamishiwa Mwanza.

Katika uteuzi wa viongozi walioteuliwa wiki iliyopita watatu walikuwa ni wakuu wa mikoa.

Ingawa Mtanda alikabidhiwa ofisi Jumapili iliyopita na Makalla, hakukuwa na tukio lolote kubwa katika mitaa ya Jiji la Mwanza. leo, Jumatatu, Jiji la Arusha lilishuhudia msafara mrefu wa magari, mengi yakiwa ni ya kiraia, yakitokea Uwanja wa Ndege wa Arusha kwenda ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha mbako shughuli ya makabidhiano ya ofisi ilifanyika.

Ingawa magari hayo mengi yalikuwa ni ya kiraia, kwa maana hiyo, gharama zake hazikuwa za serikali, kilichoonekana kinafanana na kushabihiana kabisa na ile misafara ya Makonda akiwa Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM. Hata kundi la waandishi wa habari waliofika Arusha kutoka Dar es Salaam kuripoti makabidhiano hayo, pia ni mpango wa wandani wa Makonda.

Katika nafasi ya uenezi ambayo Makonda alihudumu kwa siku 161, tangu alipoteuliwa Oktoba 22, 2023 alifanya ziara katika mikoa yote ya Tanzania. Katika ziara hizo, kila alikopita kulikuwa na misururu mirefu ya magari, ya serikali na binafsi. Katika ajali ya msafara wake iliyotokea Masasi, Mtwara Februari 11, mwaka huu, ukweli wa magari yaliyokuwa kwenye msafara wake ulidhihirika.

Jana akitokea Uwanja wa Ndege wa Arusha, ile sura ya misafara mirefu ilionekeana majira ya asubuhi. Makonda aliyewasili Arusha akitokea Dar es Salaam kwa ndege ya Precision, alilakiwa na viongozi kadhaa wa serikali wa mkoa huo. Hata katika kujionyesha katika ukwasi huo, anajiita mtetezi wa wanyonge!

Ulinganifu wa jinsi alivyofika ofisini na Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, Mtanda, ni mbingu na ardhi. Hakuna msafara wowote wa Mtanda uliyoonekana katika jiji la Mwanza, ambalo kwa ukubwa wa idadi ya watu linazidi Arusha, wala hakukuwa na ‘vibweka’ katika makabidhiano ya ofisi, mbali tu ya kuahidi kusaidiana na wakazi wa Mwanza kuirejesha ligi kuu timu maarufu ya soka, Pamba ambayo ilivuma sana miaka ya 80 na 90 ikiwa na jina la TP Lindanda.

Pengine kilichoteka masikio ya wengi ni kauli za Makonda ambazo alizitoa katika hafla ya makabidhiano ya ofisi. Alitangaza wazi kuwa “Rais Samia amemtoa mwanaye wa pekee kwenda Arusha.” Na kwamba ametumwa kama mtoto mteule kwenda kutimiza torati ya Rais Samia Arusha.

Pia alidokeza kuwa atakuwa ni kiongozi wa aina gani. Kwamba hana muda wa kubembelezana na mtumishi yeyote wa umma. Hatajali mtu yeyote kwa cheo chake, “Sitajali wewe ni nani, baba yako ni nani, ulipataje hicho cheo; aidha ulipata kwa kuhonga, ulipata kwa rushwa, ulipata kwa mganga, nitakula sahani moja na wewe.”

Makonda hakuishia hapo tu, aliongeza kuwa kuna watu wanadhani kwamba kwa kuwa ametoka kwenye nafasi ya uenzi sasa atakuwa amepoa. Alitaka kila mtu awajibike kwenye nafasi yake.

Hata hivyo, Makonda akiendelea na ile haiba yake ya kunena kama mtu mwenye mamlaka maalumu, alisema: Hana alichojifunza kutoka nafasi ya Uenezi zaidi ya kuwashughulikia wazembe, wavivu na walarushwa.

Inawezekana kabisa Makonda anao mvuto wa kipekee katika siasa za Tanzania, pia inawezekana anazungumza lugha inayoeleweka kwa wengi, hasa watu wa ngazi ya nchini ambao mwenyewe anawaita ‘wanyonge’ kwa maana hiyo, anapata kuungwa mkono nao kwa wingi.

Kadhalika, inawezekana Makonda anazungumza kile ambacho aghalabu viongozi wengi wa ngazi yake hawayasemi. Ama wanasita kuyasema kwa sababu ni mambo ambayo yamefungamanishwa kwenye mfumo wa utawala.

Akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi Makonda alitembea nchi nzima kwa kipindi cha miezi mitano alichokalia kiti hicho, alikutana na malalamiko ya kila aina kutoka kwa wananchi waliokuwa wanajitokeza kwa wingi kumsikiliza katika mikutano yake na kuwasilisha kero zao kwake. Kuna nyakati Makonda alipiga simu hadharani na kuwahoji baadhi ya mawaziri moja kwa moja, akitaka kupata majibu ya kero/shida za wananchi.

Ingawa kuna uwezekano kuwa nyingi ya shida hizi zinaweza kuchangiwa na uzembe au rushwa au uvivu tu wa watumishi wa umma, kuna jambo ambalo Makonda na wengine wa aina yake ama hawaelewi au wanafumbia macho. Mfumo wetu wa utawala umekwama kuleta matokeo chanya kwa umma.

Mfumo huu wa kuanzia serikali kuu, kwenda mkoani mpaka wilayani, ambako Rais huwakilishwa na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, ni mfumo wa mlolongo wa serikali kuu kwenda hadi ngazi ya chini kabisa. Wakati serikali kuu ikijitanua kwa mfumo huo, kuna halmashauri za wilaya au miji, au manispaa au majiji ambazo zina vongozi ambao kimsingi wanapaswa kujisimamia na kuwaletea wananchi maendeleo.

Hawa wanasimamia ardhi, elimu, afya, kilimo, miundombinu, biashara na kila eneo linalomuhusu mwananchi. Watumishi wote hawa wako chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri husika. Mkurugenzi huyu ni mkono wa serikali kuu. Uteuzi wake na utii wake ni huko huko juu!

Kwa kiwango fulani, ngazi hii ya madaraka ilipaswa kuwa imepewa madaraka kamili ya kuongoza maeneo yao, kuangalia ni kwa jinsi gani kila eneo la nchi ni la kipekee na hivyo kuibuka na mbinu za kuwaletea maendeleo wananchi wake. Hapa suala la ugatuzi wa madaraka (D by D) ni la umuhimu wa kipekee. Ni dhahiri, siyo jambo la bahati mbaya kuwa matatizo ya mikoa yote yanafanana. Kero ya ardhi (migogoro), kero kwenye elimu, huduma za afya na nyingine za kijamii. Kiini chake kikuu ni mfumo wa kiutawala. Bado mamlaka ya serikali kuu ni makubwa sana juu ya mamlaka ya serikali za mitaa. Huko chini ndiko kwenye wananchi, lakini madaraka makubwa bado yako juu. Waziri mwenye dhamana na serikali za mitaa anaweza kuvunjilia mbali halmashauri!

Nilidhani Makonda baada ya kuwa amehudumu katika mkoa wa Dar es Salaam kwanza kama Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na baadaye kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, angelikuwa ametambua kwamba mfumo wetu wa utawala unasigana mahali fulani, na msigano huo unasababisha kukosekana kwa ufanisi. Mamkala ya serikali za mitaa dhidi ya serikali kuu.

La pili ambalo nilidhani Makonda angekuwa amejifunza ni hili, haijalishi anaingia ofisini kwa mbwembwe za namna gani, hata kama wangemwandalia magari yote ya mkoa wa Arusha ili kuonyesha kuwa yapo mamlaka mapya yameingia Arusha, bado hatabadili mfumo wa utawala ulioko.

Huwezi kuwa na mfumo wa viongozi wanaohudumia wananchi lakini hawawajibiki kwa wananchi husika. Mfumo wetu bado ni wa Bwana Mkubwa ambao tuliurithi kutoka ukoloni. Serikali kuu kushuka mpaka chini kwa wananchi si kusaidia wananchi katika ngazi hiyo, bali kuirahisishia serikali kuu kutawala.

Ndiyo maana ukisikiliza vizuri sana vyeo vingine vya RC na DC ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wa maeneo yao. Yaani hawa wanakuwa ni mkono wa vyombo vya mabavu vya serikali kuu. Mkuu wa Wilaya ana madaraka makubwa na mazito kuliko Mwenyekiti au Meya wa Halmashauri, vivyo hivyo mkuu wa Mkoa.

Kwa hiyo kama watendaji wa nafasi za chini hawajali sana haki za wananchi ni kwa sababu hiyo hiyo, madaraka kamili yako juu na siyo chini. Na hili Makonda aliliona ama akiwa DC au RC na juzi juzi hapa akiwa Mwenezi wa CCM, kilio cha wananchi dhidi ya kutokujali kwa watendaji.

Lakini kama alivyosema mwenyewe kwenye uenezi hakujifunza lolote jipya mbali ya kuwashughulikia wazembe, wavivu na walarushwa, ndiyo maana sasa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameona njia ya kufanya ni kuonekana akiingia kwa mamlaka makubwa chini ya msafara mkubwa wa magari, hata kama haiwekwi wazi nani aliandaa mapokezi hayo ya magari ya kufanana na mojawapo kati yake akapanda Makonda huku akipungia watu.

Huu ndiyo ukuu anaupeleka Arusha, lakini kwa mfumo wa kutokuwa na mamlaka ya maana kwenye ngazi za chini, mabaraza ya madiwani kutokuwa na nguvu, mameya na wenyeviti wa halmashauri kutokuwa na nguvu kama wawakilishi wa wananchi, itakuwa ni miujiza kwa mabadiliko anayowaza Makonda kutokea Arusha. Mfumo wetu umekwama siku nyingi. Tufanye kweli katika dhana nzima ya ugatuzi wa madaraka

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...