DODOMAWaziri Mkuu wa Ethiopia Dkt. Abiy Ahmed Ali anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia Februari 29 – Machi 02, 2024 kwa mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Abiy na ujumbe wake watapokelewa rasmi Ikulu, Dar es Salaam tarehe Mchi 01, 2024 na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia, na wanatarajiwa kurejea Ethiopia, Machi 02, 2024.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne (Februari 27,2024) na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki imesema, lengo la ziara hiyo mbali na kukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili. “Inalenga pia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ethiopia ambazo zimekuwa zikishirikiana katika maeneo ya biashara na uwekezaji, elimu, utamaduni, usafirishaji wa anga, kilimo, mifugo, udhibiti wa uhamiaji holela, ulinzi na usalama,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Tanzania na Ethiopia zina uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wa kihistoria ambao ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mtawala wa Ethiopia, Hayati Haile Selassie.
Viongozi hawa walishirikiana bega kwa bega katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na ni miongoni mwa viongozi 32 waanzilishi wa Umoja wa Afrika (AU), wakati huo ukiitwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mwaka 1963.Mbali na ushirikiano wa kidiplomasia, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya anga ambapo mwaka 2016 hadi 2023 jumla ya marubani 75 na wahandisi 25 kutoka Tanzania wamepokea mafunzo katika ngazi tofauti nchini Ethiopia. “Hivyo ni wazi kuwa, ziara hii itafungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya Shirika la Ndege la Ethiopia na Shirika la Ndege la Tanzania – ATCL katika kujiendesha kibiashara,” taarifa hiyo imesema na kuongeza:“Kadhalika, Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika sekta ya mifugo na kilimo.
Nchi hizi zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo na uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo kama kahawa, chai, asali, mbogamboga na matunda barani Afrika.” Imesema kupitia ziara hiyo Tanzania na Ethiopia zitaimarisha ushirikiano katika masuala ya umwagiliaji, matumizi ya teknolojia katika kilimo na matumizi ya mbegu zenye ubora na uhakika wa mavuno sambamba na tafiti katika sekta hizo mbili.
Kuhusu sekta ya nishati, taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanzania na Ethiopia kujengeana uwezo na kubalishana uzoefu katika uzalishaji wa umeme unaotosheleza mahitaji ya nchi pamoja na kuzalisha umeme wa kibiashara utakaoiwezesha Tanzania kuuza nishati hiyo katika nchi mbalimbali kupitia uanachama wake ndani ya Jumuiya ya kuuziana umeme ya Afrika Mashariki (East African Power Pool).
Aidha, katika sekta ya elimu ziara hii itaziwezesha nchi hizi mbili kubadilishana wanafunzi na kujenga uwezo katika uuandaji wa mitaala na Tanzania kupata fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia.