Tuache blablaa! uandishi wa habari siyo riwaya

JUMATATU Februari 26, 2024 yaani mwanzo wa wiki hii taifa lilishuhudia jambo kubwa la kihistoria la kufanyika kwa jaribio ya safari za treni ya umeme kwenye reli ya standard gauge (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Ni tukio la kihistoria kwa maana kwamba nchi hii haijawahi kuwa na treni ya umeme, ingawa Reli ya Tazara ni ya viwango vya standard gauge.

Katika tukio kama hili, umma umetaarifiwa juu ya jaribio hilo na vyombo vya habari. Binafsi nilipata bahati ya kujua uzinduzi huo kupitia clip ndogo ya ‘repota’ wa Wasafi TV ambaye alionekana akiwa na uso wa bashasha akishangilia kufika Morogoro kwa treni hiyo, hakuripoti cha maana hata hivyo!

Nilikimbilia kwenye tovuti ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuangalia kama wameweka habari hiyo kwenye mtandao wao. Sikuona. Habari mpya ya mwisho niliyoiona kwenye tovuti ya TRC ni iliyowekwa Februari 23, 2024 ikiwa na kichwa kisemacho: Benki ya Maendeleo Afrika yatoa Bilioni 231.3 kufadhili ujenzi wa SGR kuunganisha Burundi na DRC.

Suala la kuanza kwa safari za treni ya umeme kati ya Dar es Salaam na Morogoro limekuwa na mvutano wa muda mrefu. Viongozi mbalimbali wa serikali na hata wa TRC wamekuwa wakitoa ahadi za tarehe tofauti tofauti za kuanza kwa safari hizo, bila mafanikio. Katika hali hiyo, suala la safari za treni ya umeme limekuwa ni tete.

Baada ya kuona hiyo clip jana nilibaki na maswali mengi kichwani badala ya kujua kwa kina juu ya SGR na treni ya umeme. Nilitamani kujua hali reli iko je kati ya Dar es Salaam na Morogoro? Nilitaka kujua lile eneo lililokuwa korofi na sugu kwa mafuriko sasa liko vipi baada ya ujenzi wa reli hii mpya? Nilitaka kujua kama kuna sehemu milima imetobolewa na sasa treni inazama ndani na kuibukia upande wa pili? Nitaka kujua hali ya mabehewa, je, abiria anaweza kurandaranda ndani ya treni ikiwa kwenye mwendo kasi? Nilitaka kujua hali ya umadhubuti wa treni, mabehewa, reli. Nilitamani kuona wataalam na abiria wa treni hiyo wakihojiwa ili watoe simulizi ya kina juu ya treni hii ya kihistoria kwa nchi yetu. Maswali ni mengi, lakini kizazi kipya cha ‘waandishi’ wa habari watakuhabarisha nini? Wanaitwa influencers! Achana na kuripoti.

Sikupata majibu kwa sababu moja kubwa, kuendelea kwa mtindo wa kudhani kwamba habari ni jambo la mizaha linaloweza kufanywa na kila mtu alimradi tu anajua kuzungumza. Kwao riwaya na habari ni sawa tu!

Mara nikakumbuka mtifuano uliopata kutokea katika mkutano wa waandishi wa habari na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Stergomena Lawrence Tax juu ya waandishi wa habari wa kisasa na wa kizamani. Kwamba waandishi wa habari wa kizamani walitakiwa wakae nyuma ili mbele wakae wale wa kisasa. Ambao yamkini walionekana kuwa ndio Waziri alitaka wamsaidie kubeba ujumbe wake. Influencers! Ulitokea mzozo. Si madhumuni ya uchambuzi huu kurejea mzozo ule. Itoshe tu kukumbusha kwamba sisi kama taifa ama kwa kujua au kwa kutokujua tunajizamisha kwenye mtanziko mkubwa unaohusu habari.

Nitatoa ufafanuzi kidogo. Mwandishi wa habari ni mtu gani? Mwandishi wa habari ni mtu aliyeamua kwanza kutafuta maarifa na ujuzi juu ya namna ya kutafuta na kuchakata habari kwa ajili ya watu wengine. Mtu huyu hubeba dhima ya kuhakikisha kwamba mambo muhimu kwa ajili ya ustawi wa jamii yanaripotiwa kwa weledi, kwa ukweli, uhakika na kwa njia ambayo inamfanya yule anayesikiliza simulizi au anasoma habari iliyoandikwa anakata kiu ya kujua jambo husika lilitokea kwa kina na ukamilifu.

Ndiyo! Mwandishi wa habari anatakiwa awe mtundu. Aongeze vionjo kwenye habari anayoandika, lakini kamwe kutia chumvi, kupotosha na kujisemea tu mambo bila ushahidi siyo uandishi wa habari. Inawezekana siku hizi watu wanachanganya simulizi za riwaya na uandishi wa habari. Mwandishi wa habari kazi yake ni kuhoji maswali kwa wenye majibu na kuyawasilisha kwa umma katika usahihi wake tena baada ya kuyathibitisha. Ni kazi inayohitaji utulivu wa akili, kusikiliza, kuuliza maswali kuhusu hayo yanaozungumzwa, na ikibidi kudadisi zaidi na zaidi kwa nia ya kujenga uelewa wa jambo lenyewe ili jamii inayolengwa kupelekewa habari hiyo ikate kiu ya kufahamu jambo husika kwa kina. Uandishi wa habari ni taaluma. Watu wanafundishwa mbinu za kuwa mwanahabari. Ingawa wapo wenye kipaji, lakini hata katika hicho kipaji bila kujibidiisha kusoma na kudadisi, hawezi kuwa mwanahabari wa maana kwa jamii yake.

Sasa nirejee kwenye SGR na treni ya umeme. Jana kwenye kundi sogozi la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) niliuliza wahariri wenzangu kama kilichokuwa kimeripotiwa kuhusu treni hiyo ikilikata kiu ya msikilizaji/mtazamaji kuelewa hasa hiyo safari ya majaribio ilikuwa je.

Nilikumbusha mambo kadhaa ya huko nyuma kuhusu matukio mahususi ya miradi mikubwa iliyopata kuzinduliwa hapa nchini na ilivyoripotiwa. Nilikumbusha juu ya uzinduzi wa daraja la Mkapa katika mto Rufiji. Nakumbuka kuna mwandishi na mpigapicha wa gazeti la Majira alienda kwenye tukio lile. Alirejea na taarifa za kina kuhusu lile daraja. Kwamba lina urefu gani, limechukua vifaa vya ujenzi kiasi gani kama nondo, mchanga, kokoto, sementi, ukubwa wa nguzo za daraja nk. Zilikuwa ni taarifa ambazo mtu yeyote ukisimuliwa unaweza kupata picha ya hilo daraja kwa simulizi tu ya vifaa husika kwa kina.

Tukio jingine ni lile la sakala la kubinafsishwa kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Aliyekuwa Mkurugenzi wake na baadaye Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Idris Rashid aliweka katika lugha ya picha deni la NBC kwa wakati huo miaka ya katikati ya 90. Alisema deni la NBC ni kubwa kiasi kwamba kama mtu angepanga deni hilo kwa kutumia noti za Shilingi 1,000 za wakati ule, zingefika sawa na kilele cha Mlima Kilimanjaro. Lugha hii ya picha ilimfanya kila mtu kuelewa kina cha madeni ya NBC kwa wakati huo na ni kwa nini ilikuwa ni muhimu kuibinafsisha.

Uandishi wa habari ni kusimulia kwa uhakika, ukweli kwa kina. Ni kumfikisha mtu aliyeko nyumbani kwake eneo la tukio. Huo ndio uandishi wa habari na hakuna tekinolojia itakayobadili ukweli huo hata kama upatikanaji na upashaji wa habari utarahisishwa kwa nyenzo ya maendeleo ya tekinolojia.

Hata ikitumika akili mnemba (AI) bado taarifa za kina, ukweli, usahihi havitabadilika. Ni lazima habari ikamilike kwa mantiki hiyo.

Kuna nyakati napigwa bumbuazi kila nisikiapo uandishi wa habari wa kisasa. Undishi wa kizazi kipya. Kila nikisia hivyo huwa najiuliza, je, katika muktadha wa usasa, ukweli unaondoka? Je, uelewa wa jambo kwa kina unaondoka? Je, usahihi unaondoka? Je, kutokuegemea upande wowote kunaondoka? Je, mwandishi kutokujitumbukiza kwenye habari, nako kunaondoka?

Tanzania siyo kisiwa. Tunafuatilia na kuona wengine kwenye vyombo vikubwa vya habari vya dunia hii wanavyoripoti. Tena ambao ni wa kwanza na wepesi kupokea tekinolojia hasa ya kidijitali kuliko sisi. Sijaona kokote taratibu na maadili ya uandishi wa habari yakikiukwa kwa sababu eti sasa ni rahisi mtu yeyote tu kujigeuza kuwa mwandishi wa habari.

Uandishi wa habari ni kuripoti ukweli kwa kina, kuzingatia kutoegemea upande, kupiga riwaya siyo uandishi wa habari.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...